Header Ads

Shilingi 679,400,000/= zakopeshwa kwa vijana waliomaliza vyuo vya ufundi stadi nchini

Mikopo yenye thamani ya shilingi 679,400,000/= za kitanzania imetolewa kwa vijana waliohitimu mafunzo katika Vyuo vya Ufundi Stadi vinavyotambuliwa na VETA na SIDO na wanawake wajasiriamali katika mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Njombe na Lindi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mpango wa  Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) katika kipindi cha mwezi Julai hadi Septemba, 2017.

Takwimu hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakati akiwasilisha Taarifa ya Utendaji ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) kwenye kamati hiyo.

Mhe. Mkuchika amesema kuwa, mikopo hiyo imetolewa kwa vijana wapatao 176, wanawake 641 na kundi maalumu lenye walengwa 16 ikiwa ni  mkakati wa kuwawezesha watanzania wenye kipato cha chini kuwa na miradi ya maendeleo pamoja na kuunga mkono Sera ya Uchumi wa Viwanda inayosititizwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.

Mhe. Mkuchika amefafanua kwamba, katika kipindi cha Julai hadi Septemba 2017, walengwa wa mfuko wapatao 1,145 wamepatiwa mafunzo ili waweze kupatiwa mikopo, kati ya hao, 441 walipata mafunzo ya awali, 344 walipata mafunzo endelevu na vijana 20 walioathirika na matumizi ya dawa za kulevya na biashara ya ngono walipatiwa mafunzo ya afya kwa kushirikiana na kitengo cha Afya CCBRT na Jeshi la Polisi mkoa wa Dar es Salaam.

Aidha, Mhe. Mkuchika amesema, tangu mfuko uanze kutoa huduma mpya za mikopo baada ya muundo mpya kuanzia 2014/15 mafanikio mbalimbali yamepatikana, ambapo wananchi wengi wamepata mwamko wa kuanzisha miradi endelevu ya uzalishaji mali.

Sanjari na hilo, Mhe. Mkuchika ameanisha kuwa, ubunifu wa miradi na biashara endelevu umeongezeka kwa wahitimu wa vyuo, pamoja wanufaika wameweza kutengeneza ajira mpya 250 kwa vijana na wanawake.

“Mikopo inayotolewa na mfuko imewezesha kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya uzalishaji mali ikiwa ni pamoja na usindikaji wa siagi za karanga, batiki na washonaji nguo, sabuni na dawa za usafi, ushonaji wa vikapu na bidhaa za ngozi, uchakataji takataka, na uchongaji wa vinyago” Mhe. Mkuchika amefafanua.

Mhe. Mkuchika amesisitiza kuwa, Serikali inaamini kwamba kundi la vijana na wanawake likipewa nguvu ya mtaji na elimu ya ujasiriamali litashiriki kikamilifu katika kujenga uchumi wa viwanda, kuchangia pato la Taifa, kutengeneza ajira, kupunguza umasikini na kuleta ustawi wa jamii nchini.


PICHANI JUU: Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika akiwasilisha Taarifa ya Utendaji ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) kwenye Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa.
Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika wakati akiwasilisha Taarifa ya Utendaji ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF).
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Utawala na Serikali za Mitaa, Mhe. Mwanne Ismail Mchemba (Mb) akichangia hoja mara baada ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni (Mstaafu) Mhe. George H. Mkuchika kuwasilisha Taarifa ya Utendaji ya Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF) kwa kamati hiyo.No comments

Powered by Blogger.