Header Ads

JAFO: Kuzingatia maadili na kupiga vita rushwa ndio msingi Mkuu wa Maendeleo ya Taifa

Uzingatiaji wa Maadili na mapambano dhidi ya Rushwa miongoni mwa viongozi, watumishi wa umma na wananchi ndio msingi mkuu utakaowezesha kuimarisha maendeleo endelevu nchini.

Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb) amesema hayo wakati akizindua Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Hazina Ndogo.

Mhe. Jafo amesema siku hiyo iende sambamba na uwekaji wa mkakati madhubuti wa kukabiliana na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa, ikiwa ni pamoja na kupinga matendo yasiyo ya kiuadilifu kwa baadhi ya viongozi na watumishi wa umma nchini.

“Rushwa ni adui wa haki, na kuwepo kwake kunawanyima wananchi haki ya kupata huduma bora” Mhe. Jafo amesema na kuongeza wananchi wanatakiwa kuwa na uzalendo kwa nchi yao kwa kuepuka rushwa na kuzingatia uadilifu.

“Kila mtu ajitathmini amefanya nini katika kuchangia mkakati wa mapambano dhidi ya rushwa na mpango wa kuimarisha uadilifu katika taifa letu” Mhe. Jafo amesisitiza.

Aidha, Mhe. Jafo amezindua Klabu za Maadili kumi na tano (15) zilizoanzishwa katika shule za Msingi, Sekondari na Vyuo Vikuu ili kuweza kuandaa taifa la vijana waadilifu na wapinga rushwa.

Mhe. Jafo katika tukio la uzinduzi wa klabu hizo amewaelekeza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote nchini kuratibu na kusimamia uanzishaji wa Klabu za Maadili katika shule zote za Msingi na Sekondari katika Halmashauri zao.

Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa itafikia tamati tarehe 10 Disemba 2018 na kaulimbiu yake ni “Wajibika: Piga Vita Rushwa, Zingatia Maadili, Haki za Binadamu na Utawala Bora kuelekea Uchumi wa kati”.

PICHANI JUU: Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb) akizungumza wakati wa uzinduzi wa Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Hazina Ndogo.
Sehemu ya washiriki waliohudhuria ufunguzi wa Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Hazina Ndogo wakimsikiliza mgeni rasmi, Waziri wa Nchi - Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Selemani S. Jafo (Mb)  .
Baadhi ya wanafunzi waliowawakilisha wenzao wakati wa Klabu za Maadili wakati wa wa Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa mkoani Dodoma katika Ukumbi wa Hazina Ndogo.

No comments

Powered by Blogger.