Header Ads

DK NDUMBARO: Upandishwaji vyeo serikalini uzingatie utendaji kazi

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro amehimiza suala la upandishwaji  vyeo kwa Watumishi wa Umma lizingatie utendaji kazi wa mtumishi husika na si suala la sifa ya kimuundo pekee kwa maana ya muda wa kutumikia miaka mitatu mitatu  kama wengi wanavyodhani.
Dkt. Ndumbaro  amesema hayo kwa nyakati tofauti katika Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Namtumbo na Manispaa ya Songea mjini katika ziara yake ya kikazi ya siku tano ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma, na kusisitiza kuwa mtumishi anayewajibika vizuri katika utendaji kazi wake  wa kila siku ndiye atakayepandishwa cheo na si vinginevyo.
Dkt. Ndumbaro amelazimika kutoka ufafanuzi huo, kufuatia baadhi ya watumishi katika Halmashauri hizo kulalamika kutopandishwa madaraja (vyeo) kwa wakati  kwa muda mrefu sasa wakati wenzao walioanza nao kazi wameshapandishwa vyeo, hivyo kupelekea  uwepo wa tofauti kubwa ya mishahara  baina yao .
“Haiwezekani Serikali ikapandisha mishahara kwa watumishi  wasiowajibika, walevi  na wasio na nidhamu na uadilifu  katika utendaji wao wa kazi, atakayewajibika katika utendaji wake ndiye atakayepandishwa ngazi ya mshahara”, Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Dkt. Ndumbaro ameainisha kuwa, malalamiko mengi ni ya Walimu ambao wamekuwa wakidhani kuwa kila baada ya miaka mitatu lazima wote wapandishwe vyeo (madaraja) hata kama hawajawajibika ipasavyo, suala ambalo si sahihi.
“Haiwezekani  Mwalimu anayefundisha vizuri darasani na  wanafunzi wake wanafaulu vizuri  masomo yake  akapandishwa daraja  sawasawa  na yule ambaye ufundishaji wake hauridhishi na ni mlevi wa kupindukia hali inayochangia wanafunzi wengi kutofaulu somo lake”, Dkt. Ndumbaro amefafanua.
Aidha, Dkt. Ndumbaro amesema, hivi karibuni, ofisi yake inatarajia kukutana na Tume ya Utumishi wa Walimu na kuzungumza na Walimu ili kutoa elimu na ufafanuzi yakinifu wa vigezo vya msingi vinavyozingatiwa katika   suala la upandishaji vyeo kwa watumishi wa umma  nchini  kwa lengo la kuepukana na malalamiko yasiyo ya lazima. 

Dkt. Ndumbaro anaendelea na ziara ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma katika Halmashauri ya Wilaya ya Tunduru.

PICHANI JUU: Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma.
 Baadhi ya watumishi wa Hamashauri ya Wilaya ya Nyasa wakisikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) akiwa katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma.
 Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro akisalimiana na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo mara baada ya kuwasili katika Halmashauri hiyo katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma.
 Katibu Tawala Mkoa wa Ruvuma, Bw. Hassan Bendeyeko akitoa taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro aliyewasili mkoani humo kwa ziara yake ya  kikazi ya siku tano.
Baadhi ya watumishi wa Hamashauri ya Wilaya ya Songea wakisikiliza Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro (hayupo pichani) wakati akifafanua masuala mbalimbali ya kiutumishi  katika ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji mkoani Ruvuma.  
Mkuu wa Wilaya ya Namtumbo Bi. Luckness Adrian Amlima akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa masuala ya kiutumishi kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dkt. Laurean Ndumbaro aliyewasili katika wilaya hiyo kwa ajili ya ziara yake ya kikazi.

No comments

Powered by Blogger.