Header Ads

Uhuru Kenyatta ndio Rais Mteule wa Kenya

Rais Uhuru Kenyatta ametangazwa mshindi wa urais wa marudio nchini Kenya akiwa na kura 7,483,895 sawa na 98%.
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafula Chebukati amesema kiongozi wa upinzani Raila odinga aliyesusia uchaguzi huo alipata kura 73,228 sawa na asilimia 0.96.
Bw Chebukati amesema jumla ya wapiga kura 7,616,217 kati ya jumla ya wapiga kura 19.6 milioni ambao wamejiandikisha kuwa wapiga kura nchini humo walishiriki uchaguzi huo wa Alhamisi wiki iliyopita.
Hiyo ni asilimia 38.84.
Rais Kenyatta, akihutubu baada ya kutangazwa mshindi, amewashukuru waliompigia kura.
Amesema uchaguzi uliomalizika ni ishara ya uthabiti wa demokrasia na uthabiti wa taasisi za Kenya pamoja na Wakenya wenyewe.
"Agosti 8, na sitachoka, Wakenya walirauka kupiga kura. Na siku hiyo walinichagua bila shaka. Ushindi wangu ulipopingwa Mahakama ya Juu, kwenye hukumu, mahakama haikupinga ushindi wangu wa 54%. Takwimu hazikupingwa. Kilichokosolewa ni utaratibu uliopelekea ushindi wangu," amesema.
Bw Odinga alikuwa ametarajiwa kutangaza mwelekeo kwa wafuasi wake baada ya tangazo la matokeo kufanywa na Bw Chebukati.
Taarifa zinasema ameamua kufanya hivyo hapo kesho.
Matokeo kamili ya wagombea wote kama yalivyotangazwa na Bw Chebukati
MgombeaChamaKuraAsilimia
Uhuru KenyattaJubilee7,483,89598.28
Raila Odinga (Alisusia)ODM73,2280.96
Mohamed Abduba DidaARK14,1070.19
Japheth Kavinga KaluyuMgombea wa kujitegemea8,2610.11
Michael Wainaina MwauraMgombea wa kujitegemea6,0070.08
Joseph Nthiga NyagahMgombea wa kujitegemea5,5540.07
John Ekuru AukotThirdway Alliance21,3330.28
Cyrus JirongoUDP3,8320.05
Bw Chebukati amesema anaamini uchaguzi huo ulikuwa huru na wa haki.
Mwenyekiti huyo amesema mambo aliyosema yalihitajika kufanyika kuhakikisha uchaguzi huru na wa haki yalitimizwa.
Amesema walitaka kuhakikisha kila kitu kilikuwa sawa.
"Hata tulibadilisha tarehe kutoka 17 hadi 26 Oktoba kuhakikisha tuna muda wa kutosha," amesema.
Kadhalika, amesema alikuwa na kundi la kusimamia mradi wa uchaguzi wa urais kuondoa majukumu kutoka kwa makamishna ambao walituhumiwa na baadhi ya wadau.
"Naweza kusema kwa uhakika, kwamba 26 Oktoba kabla ya uchaguzi kuanza, nilikuwa nimeridhika kwamba tulikuwa tumefanya kila kitu kuhakikisha kila Mkenya angetekeleza haki yake kikatiba," amesema.
"Na haki hii mtu anafaa kuitekeleza bila kutishiwa au kuzuiwa."
Bw Chebukati anasema alishangaa kwamba watu waliotafuta wa kushambulia walimwendea yeye.
Hata hivyo, anasema ndani ya tume nao walimwogopa.
"Hatutaweza kufurahisa kila mtu. Nimedumisha na kuheshimu sheria, kama mwanasheria ziwezi kuvunja sheria niliyojitolea kuilinda," amesema.
- BBC Swahili

No comments

Powered by Blogger.