Header Ads

Mbeya City: Mawindo Ya Ruvu Shooting Yaanza LeoDSC_0163

Siku mbili baada ya kurejea  kutoka  jijini Dar es Salaam kwenye mchezo wa VPL dhidi ya Simba Sc , kikosi cha Mbeya City Fc  leo kimeanza mazoezi  rasmi kujindaa ‘kutimuana’ na   Ruvu  Shooting  ya Mlandizi Pwani kwenye  mchezo mwingine wa  ligi hiyo jumamozi ijayo kwenye uwanja wa Sokoine jijini  hapa.

Akizungumza na mbeyacityfc.com muda mfupi uliopita, afisa habari wa kikosi hiki, Dismas Ten amesema, maandalizi kuelekea mchezo huo yanakwenda vizuri lengo likiwa ni kuhakikisha  City  inaibuka na ushindi  na kujiongezea pointi tatu muhimu hasa baada ya kuvuna pointi moja uwanja wa Taifa jumamosi iliyopita kufuatia sare ya 2-2 na vinara wa ligi, Simba SC.

Tumeanza mazoezi leo kwa ajili ya mchezo wa jumamosi dhidi ya Ruvu Shooting, ni mchezo muhimu kwetu na  hii ndiyo sababu imetufanya kuanza maandalizi na kujipanga vizuri mapema kabisa kuhakikisha tunaibuka washindi, ni wazi  utakuwa mchezo mgumu kwa sababu wapinzani wetu si ya kubeza, hatuna wasiwasi kwa sababu tutakuwa tunacheza mbele ya mashabiki wetu ambao watachagiza ushindi kwa ushangiliaji wao.

Akiendelea zaidi Ten alisema kuwa kwenye mazoezi ya leo,nyota Ayoub Semtawa,Juma Seif Kijiko na Hussein Ahmed walikosekana mazoezini kutokana na kuwa nje ya jiji la Mbeya kwa matatizo ya kifamilia, huku kiungo Mrisharo Ngassa na Zahoro Pazzi waliobaki jijini Dar baada ya mchezo wa Simba wakijumuika na wezao kujiweka fiti kwa ajili ya mchezo huo wa jumamosi.

Mrisho na Zahoro walibaki Dar baada ya mchezo wa Simba lakini tayari wamewasili Mbeya na leo  wamejumuika na wengine kwenye mazoezi ya asubuhi ingawa tumewakosa Semtawa, Kijiko na mlinda lango Hussein Ahmed ambao wako nje ya jiji kwa matatizo ya kifamilia, na imaniyangu kubwa watakuwa wamerejea baada ya siku mbili kutoka sasa.

Katika hatua nyingine Ten amedokeza kuwa mlinzi Sankhani Mkandawile aliyeteguka kidole cha mkono wa kushoto baada ya kukanyagwa na Mohamed Huessin  kwenye mchezo dhidi ya Simba jumamosi iliyopita  amefanyiwa upasuaji  na kurejeshwa kwenye sehemu yake kwa kidole hicho  kilichokuwa kimefyatuka  kabisa.


Sankhani  tutamkosa kwa majuma manne kupisha  majeraha yake ya kidole cha mkono wa kushoto, alikanyagwa na Mohamed Hussein, tukumbuke kuwa baada ya mchezo ule madaktari wetu walimfanyia matibabu ya awali na tulipofika Mbeya alilazimika kufanyiwa vipimo tena  na ikagundulika kuwa kidole chake kilifyatuka kutoka sehemu yake ya kawaida na kuhamia sehemu nyingine  hivyo ikalazimu ufanyike upasuaji ili  kurejeshwa kwa kidole hicho Dr Guydon Makulila ametufahamisha kuwa upasuaji huo umefanikiwa.

No comments

Powered by Blogger.