Header Ads

GAPCO Yapongezwa Kwa Kuimarisha Mbio Za Walemavu

Washindi wa mbio za Kilimanjaro Premium lager Marathon za kilomita 10 kwa walemavu zinazodhaminiwa na GAPCO Tanzania wakiwa wameshikilia mfano wa hundi ya Tsh milioni moja walizoshinda kila mmoja. Kutoka kushoto ni Charles Mihambo aliyeshinda mbio za wanaume wanaoendesha baiskeli za kunyonga kwa mikono, Voster Peter-mbio za baiskeli za magurudumu mawili kwa wanaume, Sophia Mkenda-mbio za baiskeli za magurudumu mawili kwa wanawake na Mpoki Ibrahim-mbio za baiskeli za kunyonga kwa mikono kwa wanawake.

Baadhi ya washiriki wa mbio za kilomita 10 kwa walemavu zinazodhaminiwa na GAPCO Tanzania, wameipongeza kampuni hiyo kwa kuwajali walemavu na kuhakikisha wanafanya vizuri katika riadha.

Pongezi hizi zinakuja siku chache baada ya kumalizika kwa mbio maarufu za Kilimanjaro Marathon ambapo GAPCO iliwadhamini washiriki zaidi ya 90. 

Mshindi wa mbio za baiskeli ya kunyonga kwa mikono kwa wanawake, Mpoki Ibrahim, alisema GAPCO wameweza kufanya jambo ambalo makampuni mengine yameshindwa. “Wametufanya tujisikie fahari kwani tunajua jinsi gani ni ngumu kuwasafirisha watu wote hawa wenye ulemavu lakini GAPCO wamefanya jambo la kipekee,” alisema.


Katibu Mkuu katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel akikabidhi Tsh milioni moja kwa Mpoki Ibrahim ambaye ni mshindi wa mbio za kilomita kumi kwa walemavu za Kilimanjaro Premium Lager Marathon zinazodhaminiwa na GAPCO Tanzania zilizofanyika Moshi hivi karibuni. Kushoto kwa Katibu Mkuu ni Mkurugenzi Mtendaji wa GAPCO Tanzania, Vijay Nair. 

 “Hii ni mara yangu ya pili kushiriki, mwaka jana nilikuwa mshindi wa tatu lakini nashukuru mwaka huu nimekuwa wa kwanza na nimejishindia Tsh milioni moja. Fedha hizi nitatumia kutunisha mtaji wa biashara yangu pale Machinga Complex Karume. Nitaongeza mtaji wangu wa maji na ninachoomba tu ni kuwa GAPCO waendelee kutudhamini mwakani,” alisema na kuyaomba makampuni mengine yaige mfano huo.

Alisema siri ya mafanikio yake ni mazoezi ya kutosha kwani yeye huendesha baiskeli yake kila siku kutoka Vingunguti hadi Karume. 

Kwa upande wake mshindi upande wa wanaume wanaoendesha baiskeli za kunyonga kwa mikono, Charles Mihambo, aliimwagia GAPCO sifa kwa kutumia sehemu ya mapato yao kuwajali walemavu. 

Alisema hii ilikuwa mara yake ya kwanza kushiriki mbio hizi na kilichomsukuma hasa ni udhamini wa uhakika wa GAPCO na pia alikuwa anafanya mazoezi kila siku huko Tabora, jambo ambalo lilimpa ari ya kushinda.

“Milioni moja niliyoshinda nimeshamtumia mke wangu Tabora nikisharudi tutakaa tupange tufanye nini kwani mimi ni mkulima na mfanyabiashara pia kwa hivyo tutawekeza katika mojawapo ya shughuli hizi,” alisema huku akiipongeza timu yote ya GAPCO kwa kufanikisha mbio hizo za kilomita 10.

GAPCO Tanzania ilitoa jumla ya Tsh milioni 10.4 ambazo ziligawiwa kwa washindi wa mbio hizo.

No comments

Powered by Blogger.