Header Ads

Young Africans Kurejea Kesho


Wawakilishi wa Tanzania bara kwenye michuano ya klabu bingwa Afrika, Young Africans wanatarajiwa kurejea nchini kesho tayari kwa maandalizi ya mchezo wa marudiano wa Raundi ya Awali Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Ngaya Club de Mde ya Comoro mwishoni mwa wiki Dar es Salaam.

Young Africans watakuwa wenyeji wa Ngaya Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya jana kuanza vizuri kwa ushindi wa mabao 5-1 kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya Awali mjini Moroni, Comoro.

Ushindi huo unamaanisha Young Africans watakuwa na shughuli nyepesi tu katika mchezo wa marudiano mjini Dar es Salaam, kwani hata wakifungwa 3-0 watasonga mbele.

Kiungo Mzambia, Justin Zulu alifungua akaunti yake ya mabao Jangwani baada ya kusajiliwa msimu huu kwa kuifungia Yanga bao la kwanza dakika ya 43.

Winga machachari, Simon Happygod Msuva akaifungia Yanga bao la pili dakika ya 45 na Young Africans ikaenda kupumzika inaongoza kwa mabao 2-0.

Mzambia mwingine, Obrey Chirwa akaifungia Young Africans bao la tatu dakika ya 59, kabla ya Mrundi, Amissi Joselyn Tambwe kufunga la nne dakika ya 65 na Mzimbabwe Thabani Kamusoko kufunga la tabo dakika ya 73.

Ngaya walijipatia bao lao la kufutia machozi dakika ya 66 kupitia kwa Said Anfane Bourah Mohammed aliyetokea benchi kipindi cha pili.

Na baada ya mchezo wa jana, Young Africans walialikwa nyumbani kwa balozi wa Tanzania nchini Comoro kwa chakula cha jioni.


Baada ya mchezo na Ngaya, Young Africans wataingia kambini kujiandaa na mchezo wa marudiano wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya mahasimu, Simba SC Februari 25, mwaka huu.

No comments

Powered by Blogger.