Header Ads

Wasomi Wapongeza Usawa Wa Jinsia Umoja Wa Afrika (AU)

Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu(AfCHPR)Sukhdev Chhatbar akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa tatu kozi ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial(Sekomu)kilichopo Lushoto mkoa wa Tanga wakati wa ziara ya masomo katika mahakama hiyo mkoani Arusha.Picha na Filbert Rweyemamu.

Mwandishi Wetu,Arusha

Wasomi nchini wamepongeza uteuzi wa majaji wawili wanawake wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu(AfCHPR)uliofanywa na Wakuu wa Umoja wa Afrika(AU) katika mkutano wa 28 uliofanyika nchini Ethiopia kuwa unaelenga kujenga usawa wa kijinsia katika chombo hicho cha maamuzi.

Mkutano huo pamoja na mambo mengine ulipitisha majina ya majaji wawili ambao ni Jaji Bensaoula Chafika kutoka Algeria na Jaji Chizumila Rose Tujilane wa Malawi ambao wataitumikia mahakama hiyo kwa kipindi cha miaka sita ijayo.

Majaji hao wanachukua nafasi zilizoachwa wazi na Jaji Fatsah Ouguergouz(Algeria) na Jaji Duncan Tambala(Malawi)ambao utumishi wao ulikoma tangu Septemba 5,2016.

Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial(Sekomu),Dk Happiness Rwejuna aliyewaongoza wanafunzi wa sheria kutembelea Mahakama hiyo yenye makao yake jijini hapa alisema uamuzi uliofanywa na AU ni mzuri na ufaa kuigwa na nchi wanachama katika uteuzi wa wanawake wenye uwezo katika nafasi za maamuzi.

“Naamini idadi ya wanawake wenye elimu ya juu wapo wengi na wanaweza kufanya kazi kwa umahiri mkubwa,isihishie katika ngazi ya AU tuu bali ishuke hadi kwa nchi moja moja kuona wanawake wana mchango muhimu katika maendeleo ya Afrika kwa ujumla,”alisema.

Majaji hao wanatarajiwa kuapishwa katika kikao cha 44 kinachotarajiwa kufanyika Machi 6,2017 jijini Arusha ikiwa ni mara ya kwanza kwa mahakama hiyo kuwa na majaji wanawake watano katika majaji 11 wa mahakama hiyo tangu ianze kazi zake mwaka 2004.

Naye Emmanuel Chipanta mwanafunzi wa mwaka tatu alisema uwepo wa mahakama hiyo una umuhimu katika kuimarisha utawala sheria kwani kumekua na makosa mengi yanayotendeka ambayo wahusika hawana budi kukabiliana na mkondo wa sheria.

Alisema uwiano wa kijinsia unatajwa katika itifaki iliyoanzisha mahakama hiyo katika ibara ya 12(2) na Ibara ya 14(3).

Kwa upande wake Mwanasheria wa Mahakama hiyo,Selemani Kinyunyu wakati akijibu hoja za wanafunzi hao waliotaka kufahamu uamuzi wan chi za Afrika kutaka kujiondoa katika Mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai alisema sula hilo lina sura mbili katika nchi zinazotaka kujiondoa na zinazotaka kubaki.
 
“Zipo nchi zinazoona mahakama hii imekua ikiwalenga viongozi wa Afrika zaidi badala ya kushughulikia jinai ulimwenguni kote hivyo kuona hamna sababu ya kuendelea kuwa mwanachama,lakini wapo wanaodhani ni muhimu kuendelea kuwepo ili kuotoa mapendekezo ya maboresho pale penye mapungufu jambo ninaloliunga mkono,”alisema

Afisa Uhusiano Mwandamizi wa Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu(AfCHPR)Sukhdev Chhatbar akizungumza na wanafunzi wa mwaka wa tatu kozi ya sheria katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial(Sekomu)kilichopo Lushoto mkoa wa Tanga wakati wa ziara ya masomo katika mahakama hiyo mkoani Arusha.
 
Wafanyakazi na wanafunzi wa sheria katika Chuo Kikuu cha Sebastian Kolowa Memorial(Sekomu)kilichopo Lushoto mkoa wa Tanga wakiwa kwenye chumba cha mahakama ya wazi katika Mahakama ya Afrika na Haki za Binadamu(AfCHPR) wakati wa ziara ya mafunzo. 

No comments

Powered by Blogger.