Header Ads

Wadau Waombwa Kushiriki Harambee Kuwezesha Wanawake Kwenye Kilimo Biashara.

 Mkurugenzi wa Mradi wa Ubunifu  Katika Maswala ya Kijinsia na Kuimarisha Uhakika wa Chakula Katika Ngazi ya Kaya, unaoendeshwa na taaisisi ya Land O Lakes, na kufadhiliwa na Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Watu wa Merekani (USAID),  Dk Rose Kingamkono (kushoto) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na harambee iliyoitishwa na taasisi hiyo kesho Alhamisi ikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake katika kilimo biashara  kupitia taasisi iliyojikita kwenye kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT). Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya CAWAT Dk. Victoria Kisyombe.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi ya CAWAT Dk. Victoria Kisyombe (Kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na harambee itakayofanyika kesho (Alhamisi) jijini Dar es Salaam ikilenga kukusanya fedha kwa ajili ya uwezeshaji wa wanawake katika kilimo biashara. Kulia ni Mkurugenzi wa Mradi wa Ubunifu  Katika Maswala ya Kijinsia na Kuimarisha Uhakika wa Chakula Katika Ngazi ya Kaya, unaoendeshwa na taaisisi ya Land O Lakes,  Dk Rose Kingamkono (kushoto)

Taasisi isiyo ya kiserikali ya Land O’ Lakes imewaomba wadau wa kilimo na biashara nchini kushiriki kwenye harambee inayolenga kukusanya fedha kiasi cha Tsh 150 milioni kwa ajili ya kuwezesha mradi wa kuwajengea uwezo wanawake waweze kushiriki kikamilifu katika kilimo biashara, inayotarajiwa kufanyika kesho Alhamisi.

Harambee hiyo inayotarajiwa kuongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa itafanyika jijini Dar es Salaam, huku kiasi cha fedha kitakachopatikana kikitarajiwa kuelekezwa katika kuijengea uwezo wa kiutendaji taasisi inayojihusisha na kuendeleza wanawake katika kilimo Tanzania (CAWAT).

Harambee hiyo imebeba kauli mbiu: ‘Wezesha kilimo biashara kwa ajili ya ajira, jamii na viwanda endelevu’.

“Mafanikio tutakayoyapata kupitia harambee hii yataiwezesha CAWAT kutoa mafunzo na kuwajengea uwezo wanawake wanaojishughulisha na kilimo hapa nchini kubadilika na kujikita zaidi katika kilimo biashara kwa maana kwamba watajengewa uwezo wa kufahamau fursa za masoko ya bidhaa wanazozalisha, kujitangaza pamoja kuwaunganisha na wawekazi wakubwa,’’ alisema Mkurugenzi wa Mradi kutoka Land O’ Lakes, Dk Rose Kingamkono.

Hatua hiyo inakuja huku takwimu zikionyesha kwamba zaidi ya asilimia 70 ya watu hapa nchini wanaishi vijijini na kwamba asilimia 98 ya wanawake wanaoishi vijijini wanajishughulisha zaidi na kilimo ambacho hata hivyo kinachangia asilimia 26 ya pato la nchi.

Pamoja na wanawake kuwa wahusika wakuu na wanatumia muda mwingi kwenye shughuli za awali za kilimo, mara nyingi wamekuwa hawafaidiki na jasho la kazi zao.Hali hii ni kwa kuwa wanaume wamekuwa wakihodhi masuala yote yanayohusiana na faida zitokanazo na kilimo kwa kuhusika zaidi mwisho wa mnyororo wa kilimo ikiwemo masoko,’’

“Ni katika mazingira kama hayo ndipo unaonekana umuhimu wa kuwekeza jitihada zetu za hali na mali katika kuhakikisha kwamba huyu mwanamke ambae hanufaiki na jasho lake licha kusota katika msimu wote wa kilimo sasa ananufaika na hili litawezekana iwapo atajengewa uwezo wa kufanya kile ambacho jamii inaamini mwanamke hawezi kukifanya yaani kilimo biashara,’’ aliongeza Dk Kingamkono katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam

Akizungumzia kuhusu taasisi ya CAWAT, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa taasisi hiyo Dk Victoria Kisyombe, alisema kwa sasa ipo kwenye mchakato wa awali wa kuanza kujitegemea yenyewe kiuendashaji bila kutegemea msaada iliyokuwa ikiupata kutoka kwenye mradi  unaohusu Ubunifu katika masuala ya kijinsia na kuimarisha uhakikaka wa chakula katika ngazi ya kaya (IGE), unaotarajiwa kuisha Machi  mwaka huu.


Kuelekea katika kujiendesha yenyewe bila kutegemea msaada tunaoupata kutoka mradi wa IGE, CAWAT tunaona kwamba tuna safari ndefu inayohitaji msaada kutoka kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili tuweze kutimiza wajibu wetu wa kuwasaidia wakina mama walio kwenye sekta hii muhimu ya uzalishaji. Tunawaomba sana  watanzania mmoja mmoja, taasisi, mashirika, balozi mbalimbali waguswe katika kusaidia hili.’’ Alisema Dk. Kisyombe.

No comments

Powered by Blogger.