Header Ads

Ranieri Asisitiza Kubaki Leicester City, Atamba Kuifunga Sevilla CF

Tokeo la picha la Claudio Ranieri on sevilla game

Sakata la kufanya vibaya kwenye michezo ya ligi kuu ya soka nchini England limeendelea kumuandama meneja wa klabu ya Leicester City Claudio Ranieri, kila anapokutana na waandishi wa habari.

Kwa mara nyingine, Ranieri amekutana na hali hiyo katika mkutano na waandishi wa habari uliohusu mchezo wa 16 bora wa ligi ya mabingwa barani Ulaya ambapo Leicester City watakua wageni Sevilla CF nchini Hispania hapo baadae.

Waandishi wa habari walimsakama kwa maswali meneja huyo kutoka Italia kwa kumuuliza mustakabli wake ndani ya klabu hiyo, lakini Ranieri aliwajibu kwa mkato kwa kuwaambia hatarajii kuondoka King Power Stadium.

Ranieri alisema kama kuondoka alipaswa kufanya hivyo mwishoni mwa msimu uliopita alipofanikisha mpango wa kutwaa ubingwa wa England, lakini aliona hakuna haja ya kufanya hivyo zaidi ya kuendelea kufanya kazi yake ipasavyo.

Alisema kwa sasa atakua kama mchoyo wa fadhila kwa viongozi na wachezaji wa Leicester City, endapo ataamua kuondoka huku ikifahamika msaada wake bado unahitajika kwa namna yoyote ile ili kuinusuru klabu hiyo.

"Kama kuondoka, ningeondoka msimu uliopita, Nilifanikiwa kutwaa ubingwa na nilishawishiwa na klabu nyingi ili nijiunge nazo, lakini nilikataa kufanya hivyo kwa maslahi ya Leicester City.
"Niliamua kufanya kazi na Leicester City kwa ajili ya kuijenga ili ifahamike duniani, na lengo hilo nimelitimiza kwa asilimia 100, kwa sasa kila mmoja anaijua klabu hii kutokana na mafanikio tuliyoyapata msimu uliopita, kazi kubwa iliyo mbele yangu ni kuhakikisha tunabaki kwenye ligi."
Kuhusu mchezo wa leo dhidi ya Sevilla CF, Ranieli alisema wapo tayari kwa kupambana, na ana uhakika wa kufanya maajabu ya kujiweka kwenye mazingira mazuri kabla ya kurudiana nchini England majuma mawili yajayo.
Alisema wamekwenda Hispania kwa ajili ya kupambana na sio kushindwa, hivyo aliwataka waandishi wa kutambua dhamira yao ambayo itawaongoza na kufikia lengo ndani ya dakika 90.
"Nimewataka wachezaji wangu wapambane kwa kila hali ili kufanikisha lengo la kufanya vizuri, tunataka tutengeneze mazingira mazuri ya kusonga mbele, na sio kusalia kwenye nafasi hii ambayo tumeipata kwa mara ya kwanza,”

“Sitakia litokee kama lililotokea juma lililopita kwa ndugu zetu wa Arsenal ama FC Barcelona, tumejifunza kutokana na makosa tuliyoyafanya katika michezo ya ligi ya England, hivyo ninawahakikishia tupo hapa kwa ajili ya kupambana.” Alisisitiza meneja huyo mwenye umri wa miaka 65.

No comments

Powered by Blogger.