Header Ads

Guardiola: Hatutarajii Majibu Mabaya Ya Vipimo Vya Gabriel Jesus


Benchi la ufundi la Man City lina matumaini ya kusikia taarifa za kutia moyo kuhusu majeraha yaliyomfika mshambuliaji wao kutoka nchini Brazil Gabriel Jesus, wakati wa mchezo wa ligi ya nchini England uliochezwa usiku wa kuamkia hii leo dhidi ya  AFC Bournemouth.

Jesus mwenye umri wa miaka 19, alishindwa kuendelea na mchezo baada ya kuumia kifundo cha mguu katika dakika ya 14.

Jopo la madaktari wa klabu hiyo ya mjini Manchester, linatarajiwa kumfanyia vipimo mshambuliaji huyo na kutoa majibu yatakayotoa mustakabali halisi.

"Tunatarajia taarifa nzuri kuhusu majibu ya vipimo atakavyofanyiwa kesho (leo), hatudhani kama atakuwa nje kwa kipindi kirefu," Guardiola aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC. 

"Tunapaswa kusubiri hadi kesho (leo) ili kupata uhakika wa jeraha lake lina ukubwa kiasi gani."

Baada ya Jesus kushindwa kuendelea na mchezo wa jana dhidi ya AFC Bournemouth, nafasi yake ilichukuliwa na mshambuliaji kutoka nchini Argentina Sergio Aguero.


Jesus, alisajiliwana Man City mwezi Januari mwaka 2017 akitokea nchini kwao Brazil alipokua akiitumikia klabu ya Palmeiras, tayari ameshafunga mabao mawili katika michezo dhidi ya West Ham na Swansea City, na anaingia katika historia ya klabu hiyo ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mawili katika michezo miwili ya mwanzo aliyocheza.

No comments

Powered by Blogger.