Header Ads

Guardiola Akubali Yaishe, Amsajili Toure Ulaya


Hatimae jina la kiungo kutoka nchini Ivory Coast Yaya Toure limesajiliwa katika orodha ya klabu ya Man City tayari kwa michezo ya ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora.

Jina la Toure halikusajiliwa mwanzoni mwa msimu huu katika michuano hiyo mikubwa barani Ulaya upande wa klabu, jambo ambalo lilizua tafrani kati ya meneja wa Man City Pep Guardiola, na wakala wa mchezaji huyo Dimitri Seluk.

Man City wamethibitisha kusajiliwa kwa jina la kiungo huyo mwenye umri wa miaka 33, kwa kuweka taarifa kwenye tovuti ya klabu, ambapo taarifa hiyo imeeleza kuwa, Toure amechukua nafasi ya Ilkay Gundogan aliye majeruhi.

Mchezaji mwingine ambaye ameongezwa kwenye kikosi cha man City kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Ulaya hatua ya 16 bora, ni mshambuliaji kutoka nchini Brazil Gabriel Jesus.

Man City wamepangwa kucheza na AS Monaco katika mchezo wa hatua ya 16 bora ya michuano hiyo, na mchezo wa mkondo wa kwanza umepangwa kuunguruma Etihad Stadium Februari 21 na kisha mchezo wa mkondo wa pili utapigwa mjini Monaco Machi 15.

No comments

Powered by Blogger.