Header Ads

Geoffrey Bonny (Babu) Afariki Dunia

Tokeo la picha la Geoffrey Bonny
Kiungo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, Geoffrey Bonny Namwandu (37) amefariki dunia usiku wa kuamkia leo baada ya kusumbuliwa na maradhi kwa muda mrefu.

Dada wa mchezaji huyo wa zamani wa Prisons ya Mbeya na Yanga SC ya Dar es Salaam, Neema amethibitisha taarifa za kumpoteza kipenzi chao baada ya kuhangaika naye kumuuguza kwa muda mrefu.

Neema amesema kwamba msiba upo nyumbani kwao mjini Mbeya ambako taratibu za mazishi zimekwishaanza.

Bonny alikuwa mchezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars enzi za kocha Mbrazil, Marcio Maximo na wengi wanamkumbuka kwa soka yake maridadi katika sehemu ya kiungo, licha ya kwamba aliibuliwa wakati umri wake umekwishaenda.

Alicheza Yanga chini ya kocha Mserbia, Profesa Dusan Kondic na akaendelea hata alipoondolewa mwalimu huyo na kuletwa Mseribia mwingine, Kostadin Papic.

Ni kati ya wachezaji walioiwezesha Taifa Stars kukata tiketi ya kucheza fainali pekee za michauno ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) zinazohusisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini mwao pekee.  

Hata hivyo, Maximo akamtema katika kikosi cha Stars baada ya fainali za CHAN nchini Ivory Coast mwaka 2009 kutokana na kuwa majeruhi.
Maumivu hayo yalimfanya aachwe na Yanga mwaka 2011 akaenda kumalizia soka yake Simrik SYC ya Nepal.     

No comments

Powered by Blogger.