Header Ads

UN Yaiomba Kenya Isimamie Kikosi Cha Kulinda Amani Darfur, Sudan


Kenya na Umoja wa Mataifa zimeafiki kuboresha uhusiano wao uliozorota baada ya kufutwa kazi kwa kamanda wa Jeshi la Kenya aliyekuwa katika kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa Sudan Kusini.

Hayo yamebainika katika kikao cha pande mbili baina ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.

Guterres amesema Umoja wa Mataifa umesuluhisha mzozo wake na Kenya na akamfahamisha Rais Kenyatta kuwa, "Kenya ni nchi muhimu katika eneo na ninahisi tunapaswa kushirikiana kwa ajili ya amani na usalama na tusahau yaliyopita."  

Amesema kutokana na imani uliyonayo Umoja wa Mataifa kwa Jeshi la Ulinzi la Kenya, KDF, umoja huo unataka Kenya isimamie kamandi ya kikosi cha Umoja wa Mataifa, Darfur magharibi mwa Sudan.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta amekubali kusahau yaliyopita na kujenga upya uhusiano na Umoja wa Mataifa.

Itakumbukwa kuwa, Kenya iliondoa askari wake katika kikosi cha kulinda amani Sudan Kusini mwaka jana baada ya kamanda wa kikosi hicho kufutwa kazi bila wakuu wa Nairobi kushauriwa.

Akizungumza na Guterres Jumapili, Kenyatta amesema uamuzi huo ulikuwa ni sawa na kuivunjia heshima Kenya pamoja na kuwa nchi hiyo iko katika mstari wa mbele katika kutuma wanajeshi wake kulinda amani katika eneo.


Mkutano wa Guterres na Kenyatta umefanyika pembizoni mwa kikao cha kilele cha viongozi wa nchi za Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa.

No comments

Powered by Blogger.