Header Ads

Rea III Kuanza Februari, 2017

Viongozi Waandamizi wa Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zilizo chini ya Wizara  wakiwa katika kikao cha maandalizi na kwa ajili ya vikao vya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini siku moja kabla ya kuanza kwa vikao hivyo.

Kaimu Kamishna  wa Nishati kutoka Wizara ya Nishati ya Nishati na Madini, Mhandisi Innocent Luoga, wa kwanza kulia akifuatiwa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Felix Ngamlagosi, na Mtaalamu kutoka Ewura wakibadilishana jambo kabla ya kikao na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

 Watendaji Wakuu wa wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Nishati na Madini wakifuatilia jambo wakati wa kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

 Kaimu Mtendaji Mkuu wa  Shirika la Madini la Taifa (STAMIZO), Mhandisi Hamisi Komba akijibu hoja ya Wajumbe wa kamati wakati wa kikao kati  ya Wizara na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini mjini Dodoma.
Imeelezwa kuwa Mradi Kabambe wa Kusambaza Umeme Vijijini Awamu ya Tatu unaosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) utaanza rasmi  kutekelezwa mwezi Februari mwaka huu.

Hayo yameelezwa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo mjini Dodoma wakati akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya  Nishati na Madini.

Ameongeza kuwa, katika utekelezaji wa Mradi huo, Serikali imepanga kuwakabidhi Wakandarasi watakaotekeleza mradi huo kwa Wabunge ili kuhakikisha kwamba mradi husika unatekelezwa kikamilifu.

Wakati huo huo, Kamati hiyo kupitia kwa Mwenyekiti wake Dotto Biteko imeipongeza Wizara ya Nishati na Madini kwa ukusanyaji wa Maduhuli kwa kipindi cha nusu mwaka na kueleza kuwa, mwelekeo wa ukusanyaji huo unakwenda vizuri.

Awali, akiwasilisha Taarifa ya Wizara ya Nishati na Madini kuhusu upatikanaji wa fedha na utekelezaji wa majukumu kwa kipindi cha nusu mwaka kwa Kamati, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini Profesa Justin Ntalikwa, ameeleza kuwa, hadi kufikia Disemba 31, 2016 Wizara ilikuwa imekusanya jumla ya shilingi bilioni 201.86 sawa na asilimia 54.46 ya lengo lililokusudiwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, mapato hayo yanatokana na vyanzo mbalimbali vikiwemo ada za kijiolojia, mrahaba, ada za mwaka za leseni, mauzo ya  nyaraka za zabuni, mauzo ya gesi asilia, tozo ya mauzo ya umeme na shughuli za utafiti wa mafuta na gesi asilia,”amesema Prof. Ntalikwa.

Aidha, akieleza utekelezaji wa majukumu ya Wizara kwa kipindi cha Julai hadi Disemba, 2016 Prof. Ntalikwa amesema kuwa, Wizara imeendelea kutekeleza miradi mbalimbali ya kimkakati kulingana na mpango wake na kuitaja miradi kadhaa ikiwemo mradi wa Kusafirisha Umeme Msongo wa kilovoti 400 kutoka iringa hadi Shinyanga  na kueleza kuwa, ulikamilika tarehe 28 Disemba,2016.

“Mradi wa Kinyerezi II wenye Megawati 240 utekelezaji wake umefikia asilimia 29 na Serikali imekwishatoa mchango wake wote wa asilimia 15 sawa na shilingi bilioni 110 na mradi huu unategemewa kukamilika mwaka 2018,” amesisitiza Prof. Ntalikwa.

Akizungumzia Mradi wa Kinyerezi I, Extension ya Megawati 185 ambao ni mwendelezo wa upanuzi wa Mradi wa Kinyerezi 1, ameeleza kuwa, mradi huo unaendelea kutekelezwa na unatarajiwa kukamilika mwaka 2018.

Akizungumzia uendelezaji wa Uchimbaji Mdogo, Prof. Ntalikwa amesema kuwa, ili kukuza utendaji wao, Wizara inaendelea na hatua za uanzishwaji wa vituo vya mfano vitano katika Wilaya za Kilwa, Mpanda, Chunya na Bukoba kwa ajili ya wachimbaji wadogo.


Ameongeza kuwa, vituo hivyo vitatumiwa na wachimbaji hao kuchenjua madini yao na kujifunza namna bora ya kuendesha migodi yao kitaalam na kwa tija zaidi.

No comments

Powered by Blogger.