Header Ads

Wananchi washauriwa kuchangamkia mradi wa REA


Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati Mhe. Charles Kitwanga, amewataka wananchi waliopo katika vijiji vinavyopitiwa na Mradi wa kuunganisha Umeme Vijijini unaosimamiwa na Wakala wa Umeme vijijini (REA) kuchangamkia fursa hiyo wakati ambao mradi huo unatekelezwa kwa kuwa gharama zake ni nafuu.

Mhe. Kitwanga aliyasema hayo jana wakati wa kikao chake na Mameneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) wa Wilaya za Lindi na Mtwara  waliokutana kwa lengo la kujadili maendeleo ya mradi wa kuunganisha umeme  Vijijini katika Wilaya za mikoa hiyo unaosimamiwa na REA, ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya namna ya kuvifikia vijijii ambavyo bado havijafikiwa na mradi huo awamu ya pili.

Aliongeza kuwa, wananchi walioko katika maeneo ya vijiji ambapo mradi wa REA awamu ya pili unatekelezwa, wanapaswa kuitumia fursa hiyo vizuri kwa kuwa gharama kubwa za kuunganisha umeme zimebebwa na serikali kwa kipindi hicho na endapo mradi huo utakapokamilika watatakiwa kulipa gaharama zote kama kawaida.

Aidha, alizitaja gharama  hizo kwa kipindi cha utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya pili  kuwa ni kiasi cha shilingi 27,000/- ikiwa ni gharama ya kuunganishwa  ambayo ni  VAT  na gharama za fomu kiasi  cha shilingi 5000/-  

Katika hatua nyingine Mhe. Kitwanga aliwataka Mameneja wa Tanesco kuhakikisha wanapunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Mikoa ya Lindi na Mtwara  na kuhakikisha wanaweka mipango endelevu ya upatikanaji wa nishati hiyo kutokana na kwamba mikoa hiyo inatarajia kuwa na uwekezaji mkubwa vikiwemo viwanda vya sementi.

Aidha, aliwataka watendaji hao kuwa wabunifu na kuongeza kasi ya utendaji katika shughuli zao ili kurejesha imani ya wananchi kuhusu shirika hilo kwa kuzingatia kwamba, nishati hasa umeme ina mchango mkubwa katika shughuli zote za kiuchumi na maendeleo ya taifa.

“ Lazima tuibadilishe Tanesco. Wananchi wanatakiwa waishangae tanesco kwa huduma nzuri na si vinginevyo. Sitaki umeme ukatike hovyo hovyo. Vaeni viatu mlivyopewa .Taswira ya tanesco lazima ibadilike”. Aliongeza Kitwanga.

Halikadhalika, aliwataka mameneja hao kuhakikisha wanakusanya madeni kutoka kwa wadaiwa wote zikiwemo taasisi za serikali na watu binafsi ili kuwezesha shirika hilo kujiendesha na kuendelea kutoa huduma kwa wananachi. Hivyo, amewataka wateja wote wanaodaiwa na  shirika hilo kuhakikisha wanalipa madeni yao ili shirika hilo liendee kutoa huduma stahiki.

Wakati huo huo, Meneja  Mwandamizi wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani, Mhandisi Mahenge Mugaya alieleza kuwa, tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika mikoa hiyo linaweza kuzuilika na kuongeza kuwa, tayari  zoezi la kubadilisha nguzo mbovu limeanza na kuwekwa mpya. Vilevile, aliongeza kuwa, katika kukamilisha zoezi hilo, tayari watumishi zaidi wameongezwa kutoka Dar es Salaam kwa ajili ya shughulli ya kubadilisha nguzo hizo.

Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Kituo cha Tanesco- Mtwara cha kuzalisha umeme katika mikoa ya Lindi na Mtwara , Mhandisi Didas Maleko,  wakati akitoa taarifa ya uzalishaji  umeme katika kituo hicho alieleza kuwa, kituo hicho kinazalisha  kiasi cha megawati 18 kutoka katika mashine tisa ambapo kila machine inazalisha kiasi cha megawati 2.
.
Katika hatua nyignine Mhe. Kitwanga alitembelea eneo la  wazi la makutano ya bomba la gesi la inchi 16  kutoka Songosongo na lile la inchi 36 linalotoka Mtwara kwenda Kinyerezi Dar es Salaam katika eneo la Somangafungu ili kuangalia maendeleo ya ujenzi wa mradi huo. Aidha, alitembelea kituo cha  kuzalisha umeme unaotokana na gesi asilia kilichopo Somangafungu ,kituo ambacho kina uwezo wa kuzalisha megawati 7.5. 

PICHANI JUU: 

Naibu Waziri wa Nishati na Madini anayeshughulikia nishati, Mhe. Charles Kitwanga katikati akisisitiza jambo wakati wa kikao na Mameneja wa Tanesco wa wilaya katika Mikoa ya Mtwara na Lindi (hawapo pichani).  Pamoja nae ni watendaji wakuu wa Tanesco Mikoa ya Lindi na Mtwara. Kikao hicho kilijadili maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme vijijini kupitia REA na namna ya kuvifikia vijiji ambavyo havijafikiwa katika utekelezaji wa mradi huo awamu ya pili.


Baadhi ya Mameneja wa Tanesco wa Wilaya katika Mikoa ya Lindi na Mtwara wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati nayeshughulikia Nishati Mhe. Charles Kitwanga  (hayupo pichani) wakati wa kikao. Mhe. Kitwanga alisisitiza ubunifu na kuhakikisha mameneja hao wanapunguza tatizo la kukatikakatika kwa umeme katika Mikoa hiyo.

 

Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalisha umeme cha Tanesco- Mtwara  Mhandisi Didas Maleko ( wa pili kulia) akimwongoza Naibu Waziri wa Nishati na Madini (Nishati) Mhe. Charles Kitwanga kuangalia mitambo inayozalisha umeme katika kituo hicho. Kwa mujibu wa maelezo ya Maleko, kituo hicho kina uwezo wa kuzalisha kiasi cha megawati 18.

Mhe. Naibu Waziri akitoka kuangalia maendeleo ya ujenzi wa bomba katika eneo la Somanga. Nyuma linaloonekana ni sehemu ya bomba la gesi la nchi 36 ambalo linaelekea  Dar es Salaam katika eneo la Kinyerezi likitokea Mtwara.Msimamizi wa Kituo cha kuzalisha umeme wa gesi asilia cha Somanga  Mhandisi Edwini Konyani (wa kwanza kulia) akimweleza jambo Naibu Waziri Charles Kitwanga alipotembelea kituo hicho kuona shughuli za uzalishaji wa umeme. Kwa mujibu wa Mhandisi Konyani, mitambo iliyopo kituoni hapo ina uwezo wa kuzalisha  kiasi cha megawati 7.5.

No comments

Powered by Blogger.