Header Ads

KUMEKUCHA: Redd's Original yawapiga msasa waandaaji wa shindano la Miss Tanzania 2014


Na Mwandishi Wetu
MAWAKALA wa mashindano ya urembo nchini wametakiwa kutafuta washiriki wenye vigezo kwa ajili ya kushiriki michuano hiyo mwaka huu na hatimaye kupata mshindi wa kitaifa “Redd’s Miss Tanzania 2014” atakayeipeperusha vyema bendera ya Tanzania kwenye fainali za dunia. 


Akizungumza katika semina ya mawakala hao iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Regency iliyoko Mikocheni jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi wa Lino Agency International, Hashim Lundenga(Pichani juu kulia), aliwataka kusaka washiriki bila ya kuwanyanyapaa wasichana kutokana na maumbile yao. 


Lundenga alisema kuwa mawakala hawapaswi kutoa maamuzi ya washiriki wakati wa mchakato wa kutafuta warembo na jukumu la kufanya hivyo litabaki kwa majaji.
Mkurugenzi huyo alisema pia mawakala wanaume wanatakiwa kuwa makini katika mchakato huo wa awali na kuhakikisha wanaendeleza maadili ya Kitanzania na kufanikisha sanaa hiyo inazidi kufanikiwa. 


“Si vizuri kuwakataa wasichana wanaotaka kushiriki kwa sababu eti wafupi au sabau nyingine…kufanya hivyo si sahihi, pia huu ni wakati mwingine kwa mawakala wanaume kuhakikisha mnavivuka viunzi kwa wasichana wanaojiandaa kuwaweka mtegoni,” alisema Lundenga. 


Aliwataka mawakala hao pia kuhakikisha wanafanya mazungumzo na makampuni na taasisi mbalimbali kwa ajili ya kusaka udhamini wa kufanikisha mashindano yao ambayo yanaania ngazi ya vitongoji, wilaya, mikoa na kanda. 

“Kuhusiana na zawadi pia mnatakiwa kuwa na makubaliano na washiriki kulingana na uwezo wako wakala…hata kama uko tayari kutoa jiko waeleze hivyo,” Lundenga aliongeza.
Aliwaeleza pia mawakala hao kwamba mdhamini mkuu wa mashindano hayo ni Redd’s Original ambayo imeahidi kutumia zaidi ya Sh. Milioni 500. Happiness Watimanywa ndiye mrembo anayetetea taji la taifa na mshindi wa pili, Latifa Mohammed pia walikuwepo jana katika semina hiyo inayotarajiwa kumalizika leo.

No comments

Powered by Blogger.