Header Ads

MAMEYA WA NORWAY WAKUTANA NA VIONGOZI WA LINDI NA MTWARA Na Nuru Mwasampeta,
Serikali ya Norway imeeleza kuwa, iliichukua takribani miaka ishirini kwa nchi hiyo kuanza kufaidika na matunda ya uwekezaji mkubwa katika sekta ya gesi. 

Hayo yalibainishwa na balozi wa Norway nchini Bi. Ingunn Klepsvik alipokuwa akizungumza katika ziara ya Mameya toka nchi hiyo mjini Lindi ikiwa ni sehemu ya kutoa uzoefu iliyoupata baada ya kuingia katika uchumi huo mkubwa.

Bi. Ingunn alisema tangu kuwepo ugunduzi wa gesi katika miaka ya 1960 iliwachukua miaka 20 kuanza kuzalisha gesi ambapo uzalishaji ulianza miaka ya 1980 na kurudisha gharama za uwekezaji kwa miaka ishirini, na hivyo kuchukua kipindi cha jumla ya takribani miaka arobaini hadi walipoanza kunufaika na rasilimali hiyo ya gesi.

Aidha,  mameya wa miji ya Alstahaug na Hammerfest  walisistiza umuhimu  wa kuwepo na mipango madhubuti ambayo itawawezesha wazawa kunufaika ikiwemo pia mikakati itakayowabana wawekezaji ili kuhakikisha kuwa eneo linalochimbwa  rasilimali hiyo pia linanufaika ili wananchi waweze kunufaika na uwepo wa  rasilimali hiyo.

Kwa upande wake Meya wa mji wa Alstahaug Bw. Bard Anders, alieleza kuwa nchi ya Norway iliwekeza zaidi katika elimu lengo likiwa kupata watendaji wazuri katika sekta za gesi na mafuta.

Vilevile alieleza kuwa, wanaamini kuwa kwamba wananchi wakielimishwa ni rahisi kwao kushiriki kikamilifu katika masuala ya maendeleo lakini pia hali hiyo itawajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo na mipango endelevu juu ya namna ya kuboresha vipato vyao.

Akizungumzia kuhusu namna uchumi wa gesi ulivyoinufaisha nchi hiyo kielimu, Bw. Bard alieleza kuwa, nchini Norway elimu inatolewa bure  kwa elimu ya awali na sekondari  ambapo watoto kuanzia mwaka mmoja hadi sita wanapelekwa katika shule za awali kabla ya kujiunga na  shule za msingi  na sekondari.

Akizungumzia kuhusu elimu ya juu, alieleza kuwa, elimu hiyo nchini Norway inatolewa kwa mkopo toka serikalini ambapo aliyekopa anarejea baada ya kuanza kazi.  ‘‘Watu wote Norway wanahaki sawa ya kupata elimu’’ alisisitiza Bard.

Katika ziara hiyo ujumbe huo uliishauri Serikali ya Tanzania kuwa na sera zinazowabana wawekezaji ikiwemo pia kuhakikisha kunakuwa na asilimia nyingine ya mapato inayobaki kwa ajili ya  kusaidia  kuboresha huduma mbalimbali katika eneo husika kwa  kuzingatia vipaumbelea vya wananchi  ikiwemo miundombinu, elimu, afya pamoja na kuinua hali ya maisha ya wananchi  wa eneo husika.

Kwa upande wa viongozi wa mikao ya Lindi na Mtwara waliupokea ushauri wa ujumbe huo na kujadiliana pamoja masuala mbalimbali kuhusu namna watakavyoweza kushiriki na kunufaika na rasilimali ya gesi iliyogunduliwa katika maeneo yao.

Pamoja na kujadili masula ya gesi na mafuta ujumbe huo ulipata fursa za kutembelea mashamba ya samaki yanayoendelezwa  na wananchi wa Lindi pamoja na chuo cha Ufundi Veta kinachotarajiwa kuelimisha wananchi wa mtwara juu ya masuala ya uvuvi na kuogelea pamoja na ufundi mwingine.

PICHANI JUU:

Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Lindi Bw. Nasoro Hamid akizungumza na ujumbe toka Norway ulipofika ofisini kwake kwa lengo la kubadilishana uzoefu juu ya namna  nchi hiyo ilivyoweza kunufaika  kwa  kuwekeza katika sekta ya gesi  mnamo miaka ya 1970. Anayesaini kitabu ni Bw. Alaf Jakobson Meya wa mji wa Hammerfest nchini Norway.

No comments

Powered by Blogger.