Header Ads

KAMISHNA WA SENSA YA WATU NA MAKAZI ASISITIZA MATUMIZI YA TAKWIMU SAHIHI

Ofisi ya Taifa ya Takwimu imewataka wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, siasa na waandishi wa habari kutumia takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wanapotekeleza majukumu yao.


Akizungumza na waaandishi wa habari pamoja na wadadisi wa Madodoso ya utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi  mwaka 2014 kutoka kanda ya kaskazini leo jijini Tanga Kamishna wa Sensa ya Watu na makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said amesema kuwa  ni jukumu la kila mtendaji katika eneo lake kuhakikisha kuwa anatumia  takwimu sahihi zinazotolewa na Ofisi hiyo.

Amesema  Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye mamlaka na dhamana ya utoaji wa takwimu za masuala mbalimbali nchini na kuongeza kuwa matumizi ya takwimu zisizo sahihi yana athari kwa jamii hasa wakati wa kupanga mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya vijiji mpaka taifa.

Amesema kuwa takwimu sahihi huwezesha utekelezaji wa mipango ya maendeleo na kuongeza  kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo ufumbuzi wake unaweza kupatikana kwa kufanya rejea ya takwimu sahihi kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

“Takwimu ni muhimu sana katika kupanga namna ya kukabiliana na matatizo na majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii kama mafuriko, njaa, masuala ya ardhi na elimu ambayo kimsingi yanahitaji matumizi ya takwimu sahihi  ili kujua kiwango halisi cha ukubwa wa tatizo na namna ya kupata suluhisho la kudumu kwa wananchi husika.

Amesema ni vema wadau wanaotumia takwimu kwenye majukwaa mbalimbali na waandishi wa habari kujenga tabia ya kuwasiliana na Ofisi ya Taifa ya Takwimu kabla ya kutoa takwimu walizonazo ili kupata ukweli wa hali halisi.

“Natoa wito kwa wadau mbalimbali na waandishi wa habari kuhakikisha kuwa mnapata takwimu sahihi hata kama mmezipata kutoka kwa viongozi, tafadhali hakikisheni  mnapitia mamlaka husika kupata ukweli wa takwimu hizo ili kuepuka kutoa takwimu zisizo sahihi”, Amesisitiza Kamishna wa Sensa.

Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu ikiwa ni moja ya chanzo sahihi cha habari katika masuala yote yahusuyo takwimu na rejea sahihi na kuongeza kuwa takwimu zote zinazotumika kutengeneza sera za taifa za mipango ya maendeleo zinatoka katika chanzo kimoja tu ambacho ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu.

Katika hatua nyingine Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said ametoa wito kwa Maofisa wa Takwimu walio katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kutumia vikao mbalimbali vinavyofanyika katika Halmashauri na mikoa kutoa elimu ya matumizi ya takwimu zilizopo ili waweze kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na kutatua kero mbalimbali za wananchi.

Amesema takwimu zilizopo lazima zitafsiriwe na jukumu hilo lazima lifanywe na wawakilishi hao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu walio katika mikoa mbalimbali nchini na kuongeza kuwa wataalam hao kwa kushirikiana na viongozi wengine wa halmashauri wana jukumu la kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya jamii hasa vijana ili waweze kujiajiri na kutumia fursa zilizopo katika maeneo yao ili kupunguza utegemezi.

“Naomba mtumie vikao hivyo vya hamashauri kutoa elimu kwa sababu tayari ninyi mnazo takwimu, vikao vya halmashauri huwa vinahusisha viongozi mbalimbali wa Serikali na jamii hivyo mnaweza kabisa kushauri na kushawishi kwa viongozi hao kutumia takwimu sahihi ili kuondoa matatizo mbalimbali likiwemo tatizo la ajira kwa vijana na kuondoa utegemezi kwa kuwajengengea uwezo vijana wasio na ajira kujiajiri wenyewe”, amesema Kamishna.

Aidha ametoa wito kwa watafiti na wadadisi wa Madodoso ya Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi  2014 watakaoendesha zoezi la utafiti wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi kutoa elimu kwa vijana ambao hawana kazi katika maeneo yote watakayopita ili kuwajengea uwezo wa kufanya kazi pia kuwashauri kujiunga na vyuo vya ufundi Stadi (VETA) vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kujiajiri na kuondoa wimbi la utegemezi.

PICHANI JUU: Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati) akizungumza na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kaskazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara. Kulia kwake ni Opio Mamu Msimamizi wa mafunzo katika kanda hiyo na kushoto kwake ni Juma Shaban Meneja Takwimu, Ofisi ya Taifa ya Takwimu mkoa wa Manyara.


 Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wakimsikiliza kwa makini Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (hayupo pichani) katika mafunzo ya utafiti huo yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga.

Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014 kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara wakimsikiliza kwa makini Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (hayupo pichani) katika mafunzo ya utafiti huo yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga.

No comments

Powered by Blogger.