Header Ads

MAPATO TAMASHA LA KRISMAS KUTUMIKA KITUO CHA WASIOJIWEZA

WAANDAAJI wa Tamasha la Krismas wametangaza kuwa asilimia 80 ya mapato yatakayokusanywa kwenye tamasha hilo mwaka huu yatatumika kwenye ujenzi wa kito cha wasiojiweza Pugu, Dar es Salaam.
 
Tamasha la Krismas linaloandaliwa na Kampuni ya Msama Promotion ya jijini Dar es Salaam, ambayo pia huandaa Tamasha la Pasaka kila mwaka linatarajiwa kufanyika Desemba 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
 
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari leo jijini Dar, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Alex Msama ilieleza kuwa asilimia nyingine 20 itatumika kulipia ada yatima wanaosoma shule mbalimbali hapa nchini.“Asilimia 80 ya mapato tutaipeleka kwenye ujenzi wa kituo chetu cha wasiojiweza tunachotarajia kukijenga Pugu, Dar es Salaam, huwa hatubahatishi tunapodhamiria jambo letu,” alisema Msama.
 
Kwa mujibu wa Msama, hivi sasa wanasubiri hati kutoka Wizara ya Ardhi kuhusiana na umiliki wa eneo hilo na kwamba suala hilo litakapokamilika ndipo mchakato wa ujenzi utakapoanza na wana imani jambo hilo halitachukua muda mrefu.
 
Alieleza kuwa wakati wananzisha tamasha hilo mwaka 2000 dhamira yao ilikuwa kila mwaka kusaidia wasiojiweza.“Niwashukuru wadau mbalimbali waliotusaidia kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na mpaka sasa tuna karibu Sh milioni 120, ambapo gharama nzima ya ujenzi ni kati ya Sh milioni 800 hadi Sh bilioni moja utakapokamilika.
 
“Dhamira yetu ni kuwa na kituo ambacho kitasaidia Watanzania wa mikoa mbalimbali ambao hawana uwezo katika masuala ya mavazi, elimu, vyakula na mengine mengi,” alisema Msama.  Alieleza kuwa Kamati ya Maandalizi ya Tamasha la Krismas imeamua lifanyike Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Desemba 25 na siku inayofuata watatazama mkoa gani waupe heshima.

 Alisema hilo litakuwa tamasha kubwa la nyimbo za kumsifu Mungu na litakuwa na tofauti kubwa iilinganisha na matamasha mengine yaliyowahi kuandaliwa na kampuni yake.

No comments

Powered by Blogger.