Header Ads

Redd’s Uni-Fashion Bash yazinduliwa Dar

KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chake cha Redd’s Original imezindua tamasha la mitindo na ubunifu kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu hapa nchini, litakalojulikana kama ‘Redd’s Uni-Fashion Bash’.

Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika Dar es Salaam jana, Meneja Masoko wa TBL, Fimbo Butallah alisema,  tamasha hilo lenye lengo la kuinua vipaji vya wanafunzi katika tasnia ya mitindo, linatarajiwa kuanza mwezi huu na kumalizika mwezi ujao.

Butallah alisema, tamasha hilo kwa sasa litashirikisha vyuo vyote vya elimu ya juu vilivyopo katika Mikoa ya Dar es Salaam, Iringa, Kilimanjaro na Mwanza.

“Tunataka kuinua vipaji vya wanafunzi wa vyuo katika tasnia ya mitindo, kupitia maonyesho yakatakayofanywa na wanafunzi wa vyuo hivyo, hapa tunataka wale wenye ubunifu kuonyesha ubunifu wao wa mitindo, hivyo hii ni fursa kwao kujitangaza na kudhihirisha uwezo wao,” alisema Butallah.

Kuhusu ushiriki, Butallah alisema, kutakuwa na fomu maalumu zitakazosambazwa katika vyuo husika, ambapo wanafunzi wanamitindo na wabunifu watazijaza na majaji watazipitia na kupata wabunifu 10 na wanamitindo wa idadi hiyo kutoka kila mkoa, ambao watapata fursa ya kuonesha mavazi yao siku ya tamasha.

Kuhusu zawadi, Meneja Habari na Mawasiliano wa TBL, Edith Mushi alisema, kutakuwa na zawadi mbalimbali kutoka Redd’s Original, ambapo washindi watano wa ubunifu na idadi kama hiyo ya wanamitindo kutoka kila mkoa watajiondokea na fedha taslimu.

Edith alisema, kwa upande wa wabunifu mshindi wa kwanza ataondoka na Sh 700,000 wa pili Sh 500,000 watatu Sh 300,000 huku wa nne na watano kila mmoja akiondoka na Sh 100,000.

Kwa upande wa wanamitindo mshindi wa kwanza atajiondokea na Sh 500,000 wa pili Sh 400,000 wa tatu Sh 300,000 wakati wanne na watano wakipata Sh 100,000 kila mmoja.

“Tuna imani kubwa zawadi hizi zitaongeza chachu kwa wabunifu na wanamitindo kuendeleza fani hii ya mitindo. Lakini matamasha haya pia yatahusisha burudani za aina mbalimbali za kuvutia.

“Hii itakuwa sehemu muhimu ya kuwakutanisha wanafunzi wa vyuo na kada mbalimbali katika kufurahia na kubadilishana mawazo juu ya masuala ya ubunifu na mitindo, kwani kinywaji cha Redd’s Original kimekuwa mstari wa mbele katika kuendeleza tasnia ya urembo, ubunifu na mitindo hapa nchini,” alisema Edith.

Kinywaji cha Redd’s Original pia ndicho kinachodhamini shindano la Redd’s Miss Tanzania na kinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
PICHANI JUU: Meneja masoko wa TBL Fimbo Butallah akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar Es Salaam kwenye uzinduzi wa mashindano ya ubunifu na mitindo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu nchini ( Redd's Uni-Fashion Bash 2013) yatakayofanyika katika mikoa ya Dar Es Salaam, Mwanza, Iringa na Kilimanjaro..
Kushoto ni Meneja mawasiliano na habari wa TBL Edith Mushi.
 
 Fomu zenyewe ziko hivi...
Na ufafanuzi zaidi ukatolewa...

No comments

Powered by Blogger.