Header Ads

NENO LA LEO; NYANI HATA AKIZEEKA HAACHI HULKA YAKE..

Ndugu zangu,

Katika ulimwengu huu kuna tabia na hulka. Hivi viwili vina tofauti. Kuna sifa na uwezo, navyo ni viwili tofauti.

Tabia ya mwanadamu yaweza kubadilika, lakini si hulka yake. Na mwanadamu anaweza kuwa na sifa za kufanya jambo lakini akakosa uwezo, na kinyume chake. Na kibaya zaidi ni pale majungu na fitna yanapogubika sifa na uwezo wa mtu. Kwamba badala ya mwanadamu kupimwa kwa sifa na uwezo wake, majungu na fitina dhidi ya mwanadamu huyo yanawekwa mbele na hivyo kufanywa kuwa kipimo.

Ndio, kuna wanadamu wenye kuishi kwa kupika majungu na fitna dhidi ya wanadamu wenzao. Tofauti na tabia, hizo ni hulka za wanadamu hao, haziwezi kubadilika.

Ndio, nyani hata akizeeka haachi hulka yake. Kupalamia miti ni hulka ya nyani. Hivyo, nyani hata akizeeka, hafikiri hata siku moja kukaa chini ya mti na kupumzika, atahakikisha anapalamia hata mti mfupi wa mpapai, alimradi akae juu ya mpapai. Hapo atajiona ametimiza unyani wake.

Naam, Wahenga walitwambia; kiumbe mzito.  Mwenyezi Mungu ametuumba wanadamu kwa usawa kwenye mambo mengi. Wala hakutaka kubagua; ona unyayo wa mwanadamu, uko sawa, iwe kwa tajiri au masikini.

Wewe na mimi tumepata, ama wenyewe au  kusikia mtu akilalamika kuwa soli ya kiatu chake imechakaa, kwamba anakwenda kwa fundi viatu kubadilisha soli. Lakini, wewe au mimi hatujapata kumsikia mwanadamu mwenzetu akilalamika kuwa unyayo wake umechakaa, anataka kwenda kwa fundi awekewe unyayo mwingine!

Ndio, wewe na mimi ama tumeshuhudia au kusikia kuwa upepo umeangusha mti, nyumba, ghorofa, gari na hata meli. Lakini, jiulize, je, umepata kumwona mwanadamu mwenzako anayetembea kwa miguu akiangushwa kwa upepo?

Kamwe mwanadamu haangushwi na upepo, hata awe mwembamba kiasi gani. Na ukimwona mwanadamu mwenzako anayumba na kuanguka barabarani, basi, ama ni mgonjwa, au ni mlevi. Na hilo la mwisho haliwezi kuwa na maana ya mwanadamu huyo kaangushwa na upepo, bali kaangushwa na  pombe zake alizokunywa.

Naam, kiumbe mzito.

Ni Neno La Leo.

Maggid.
Dar es Salaam.

No comments

Powered by Blogger.