Header Ads

KIKAO CHA 23 CHA BODI YA TAIFA YA PAROLE CHAANZA LEO EDEMA HOTEL, MOROGORO


Mkuu wa Sekretarieti ya Taifa ya Parole, Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, Dkt. Juma Malewa(wa kwanza kushoto) akifuatilia majadiliano ya Wafungwa watakaoachiliwa kwa Parole(wa kwanza kulia) ni Mkuu wa Kitengo cha Parole, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Magereza, Clement Keenja(Picha zote na Lucas Mboje wa Jeshi la Magereza). photoMwenyekiti wa Bodi ya Taifa ya Parole, Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo(kushoto) akiongoza kikao cha kujadili Wafungwa waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole(kulia) ni Katibu wa Bodi ya Taifa ya Parole, Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Casmir Minja. Kikao hicho cha siku mbili kimeanza leo Oktoba 3, 2013 katika Hoteli ya Edema, Morogoro.
…………………………………………………………………

Na; Inspketa Lucas Mboje, Morogoro
Kikao cha 23 cha Bodi ya Taifa ya Parole kitakachofanyika kwa siku mbili chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo kimeanza leo Oktoba 3, 2013 katika Ukumbi wa Hoteli ya Edema ambapo kikao hicho kitajadili  Wafungwa waliopendekezwa na waliopendekezwa kuachiliwa kwa Parole.

Kufanyika kwa kikao hiki ni utekelezaji wa Sheria ya Parole ya Mwaka 1990 ambayo inalenga kupambana na uhalifu nchini na hivyo kudumisha Usalama wa jamii kwa ujumla.

Dhana hii ya Parole ambayo huishirikisha jamii katika kufanikisha Urekebishaji wa wale wanaopata msamaha wa Parole tayari imekwishatumika duniani kwa zaidi ya miaka 300 na imethibitika kwamba ni mfumo sahihi katika kuimarisha Urekebishaji wa Wahalifu na hivyo kuimarisha Usalama wa Jamii.

Ipo dhana kuwa kuanzishwa kwa mfumo huu hapa nchini Tanzania ni kuweka rehani dhamana Kuu ya kudumisha Usalama wa jamii. Ukweli ni kuwa Sheria hii ya Parole haipo ili kulegeza misingi ya Usalama wa raia.

Hivyo jamii yote kwa ujumla inapaswa kuielewa na kuikubali dhana hii ya Parole na kuachana na tabia ya mtindo wa kumpeleka kila mkosaji gerezani kwani tabia hii husababisha Magereza mengi kufurika na kuwa na msongamano usioruhusu utekelezaji wa programu za Urekebishaji, achilia mbali matatizo mengineyo mengi yatokanayo na hali ya Msongamano.

Kutokana na hali hii iliilazimu Jumuiya ya Kimataifa kupitisha suala zima la Adhabu mbadala wa kifungo kuwa ni miongoni mwa maadhimio mawili ambayo kimsingi yanahimiza matumizi ya adhabu mbadala wa kifungo kama njia ya kuwarekebisha Wahalifu wa kawaida na kuyaacha Magereza yatumike kwa Wahalifu wenye kutishia Usalama wa jamii.

Hiki ni kikao cha pili kufanyika chini ya Uenyekiti wa Mhe. Jaji Mstaafu Eusebia Munuo tangu ateuliwe rasmi na Mhe. Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kuwa Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taifa ya Parole kuanzia  tarehe 24 Aprili, 2013.

No comments

Powered by Blogger.