Header Ads

IRAN YAPANGA KUANZISHA USAFIRI WA NDEGE WA MOJA KWA MOJA HADI NEW YORK

Gazeti la Tehran Times Daily la Iran limesema kuwa, njia ya kwanza ya usafiri wa ndege wa moja kwa moja kutoka Iran hadi Marekani baada ya ushindi wa mapinduzi ya kiislamu yaliyotokea nchini humo mwaka 1979, itaanzishwa hivi karibuni. 

Gazeti hilo limemnukuu ofisa wa Baraza la biashara la Iran Bw. Abolfazl Hejazi akisema, Iran imepanga kuanzisha usafiri wa ndege kutoka kisiwa cha Kish hadi jiji la New York, Marekani, na tayari hatua za mwanzo zimekamilika, na kinachosubiriwa sasa ni idhini ya shirika la usafari wa ndege za abiria. 

Baada ya mapinduzi ya kiislamu mwaka 1979, shirika la ndege la Iran lilifanya safari yake ya mwisho ya moja kwa moja kutoka Tehran hadi New York. Marekani ilivunja uhusiano wa kidiplomasia na Iran kufuatia mzozo wa utekeji nyara uliotokea mwaka 1980 mjini Tehran. 

Hivi karibuni, baada ya rais mpya wa Iran Hassan Rouhani kuhudhuria mkutano wa Baraza kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, alitoa ahadi kwa raia wa Iran wanaoishi Marekani kuanzisha usafiri wa ndege wa moja kwa moja kati ya nchi hizo mbili ili waweze kurudi nyumbani kwa urahisi.

No comments

Powered by Blogger.