Header Ads

BUNDUKI MARUFUKU UWANJA WA TAIFA, VIINGILIO MECHI ZA SIMBA NA YANGA WIKIENDI HII HII VYATAJWA

Na Boniface Wambura,
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) kupitia Jeshi la Polisi kuanzia sasa halitashikilia silaha za washabiki, na badala yake litawazuia kabisa kuingia viwanjani wakati wa mechi.

Jeshi la Polisi limekuwa likihifadhi silaha za washabiki wanaokwenda viwanjani, na baadaye kuwarejeshea baada ya mechi kumalizika kwa vile Kanuni za Usalama Viwanjani za Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinakataza silaha viwanjani.

Wikiendi iliyopita katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Jeshi la Polisi lilikamata bastola 17 katika upekuzi wa washabiki waliokwenda kushuhudia mechi kati ya Yanga na Ruvu Shooting na ile kati ya JKT Ruvu na Simba.
Iache nyumbani kesho; Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj Ismail Aden Rage atalazimika kuacha bunduki yake nyumbani kesho akienda Uwanja wa Taifa 
 
Wote waliokutwa na silaha hizo walikuwa na leseni za kuzimiliki. Hivyo, kwa washabiki wanaomiliki silaha hatawaruhusiwa kabisa kuingia viwanjani, na badala yake wanashauriwa kuzihifadhi huko wanakotoka kabla ya kufika viwanjani.

Pia TFF inatoa mwito kwa shabiki ambaye atamuona mwenzake akiwa na silaha uwanjani kutoa taarifa kwa mamlaka husika likiwemo Jeshi la Polisi ili aweze kuchukuliwa hatua.

Wakati huo huo; Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inaingia raundi ya saba kesho (Oktoba 5 mwaka huu)  kwa mechi nne ambapo Ruvu Shooting itakuwa mwenyeji wa vinara Simba kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Viingilio katika mechi hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Mohamed Theofil kutoka Morogoro kuanzia saa 10 kamili jioni vitakuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000. Tiketi zitauzwa uwanjani kuanzia saa 4 asubuhi.

Mechi nyingine za kesho ni JKT Ruvu itakayoumana na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam huku Coastal Union ikiwa mwenyeji wa Azam kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Uwanja wa Kumbukumbu ya Sheikh Kaluta Amri Abeid jijini Arusha ndiyo utakaotoa fursa kwa timu za Oljoro JKT na Mbeya City kuoneshana ujuzi katika kusaka pointi tatu.

Ligi hiyo itaendelea Jumapili (Oktoba 6 mwaka huu) kwa mechi kati ya Yanga na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam wakati Mgambo Shooting itaialika Tanzania Prisons kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.

Nayo Ligi Daraja la Kwanza (FDL) kuwania tiketi za kucheza Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) msimu ujao (2014/2015) inaendelea wikiendi hii (Jumamosi na Jumapili) kwa kuzikutanisha timu 20 zitakazopambana katika viwanja kumi tofauti.

Jumamosi kutakuwa na mechi kati ya Green Warriors na Friends Rangers (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi), Kimondo na Burkina Faso (Uwanja wa CCM Vwawa, Mbozi), Mlale JKT na Mkamba Rangers (Uwanja wa Majimaji, Songea) na Kurugenzi dhidi ya Polisi Morogoro (Uwanja wa Wambi, Mafinga).

Polisi Dodoma na Stand United (Uwanja wa Jamhuri, Dodoma), Toto Africans na JKT Kanembwa (Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza), Mwadui na Polisi Mara (Uwanja wa Kambarage, Shinyanga) na Polisi Tabora na Pamba (Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, Tabora).

Keshokutwa (Jumapili) kutakuwa na mechi kati ya African Lyon na Transit Camp (Uwanja wa Mabatini, Mlandizi) na Villa Squad dhidi ya Polisi Dar es Salaam (Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es Salaam).

No comments

Powered by Blogger.