Header Ads

AU WATAKA VIONGOZI WA NCHI WALIO MADARAKANI WASIFIKISHWE ICC

Viongozi waliohudhuria mkutano maalum wa Umoja wa Afrika wamesema kwa sauti moja kwamba, mahakama ya kimataifa ya makosa ya jinai ICC haiwezi kuwafungulia au kuendelea na mashtaka dhidi ya viongozi wa nchi za Afrika walio madarakani. Viongozi hao pia wanaitaka ICC iahirishe kesi ya Uhuru Kenyatta. 

Akihutubia ufunguzi wa mkutano huo, mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini-Zuma anaona Kenya inakabiliwa na changamoto kubwa ya kiusalama, kwa hiyo sasa si wakati mwafaka kwa ICC kuendelea na mashtaka dhidi ya viongozi wa nchi hiyo. Akisema

"Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa na ICC zinatakiwa kushirikiana na sisi, ili kuwawezesha viongozi wa Kenya waliochaguliwa na wananchi wao kutimiza wajibu na majukumu yao kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo. Kutokana na wazo hili, na kwa mujibu wa kifungo cha 16 cha Mkataba wa Roma, ICC inatakiwa kufikiria kuahirisha mashtaka dhidi ya rais na naibu rais wa Kenya." 

Baada ya majadiliano ya siku nzima, mwenyekiti wa zamu wa Umoja wa Afrika, ambaye pia ni waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Dessalegn, anasema washiriki wote wa mkutano huo wamekubali kwamba, wakuu wa nchi walio madarakani wanatakiwa kuwa na kinga dhidi ya mashtaka ya ICC. Akisema: 

"Tunaona kuwa, kama mkuu wa nchi na kiongozi wa serikali bado wako madarakani, mahakama yoyote ya kimataifa au mahakama yoyote maalum haiwezi kuwafungulia au kuendelea na mashtaka dhidi yao." 

Kesi zote nane zinazosikilizwa na ICC hivi sasa ni za nchi za Afrika, zikiwemo, Kenya, Sudan, Libya, Mali, Uganda na kadhalika, hali ambayo imezifanya nchi za Afrika kuilaumu mahakama hiyo kwa kuwaonea waafrika.

No comments

Powered by Blogger.