Header Ads

ZIARA YA VIONGOZI WA CCM WILAYA YA MAKETE YAZIDI KUIBUA MENGI

Viongozi wa CCm wilaya ya Makete wakikagua chumba cha darasa wanachosomea wanafunzi wa darasa la tatu na la nne kwa pamoja
 Katibu wa CCM wilaya ya makete Miraji Mtaturu, mwenyekiti Francis Chaula na diwani wa kata ya Kitulo Mbosa Tweve wakisikiliza maelezo kutoka kwa mkuu wa shule ya msingi Nkenja Hester Mahenge ofisini kwake
 Viongozi wa CCM wakikagua ujenzi wa madarasa unaodaiwa kusuasua, mwenyekiti wa CCM wilaya ya makete (katikati) akizungumzia ujenzi huo
 darasa wanalotumia wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kusomea

 Vyumba viwili vya madarasa ambavyo vinafaa kwa matumizi shuleni hapo
 Majengo ya shule ya msingi Nkenja, kulia na kushoto ni vyumba vya madarasa, katikati ni ofisi ya mwalimu mkuu.


Madarasa ambayo hayajakamilika lakini yanatumiaka kwa ajili ya darasa la kwanza na la pili.
Turubai likining'inia kwenye chumba ambacho wanasomea wanafuzni wa darasa la kwanza na la pili ambalo hulitumia kama bati kuzuia jua.


Na Edwin Moshi, Makete
 
Mazingira magumu hasa kwa elimu ya msingi nchini bado yanazidi kuonekana baada ya shule ya msingi Nkenja iliyopo kata ya Kitulo wilayani Makete mkoani Njombe kuonekana ina vyumba viwili tu vya madarasa ambavyo vina hadhi ya kutumiwa kama madarasa

Hali hiyo si imeacha hoi mtandao huu tu bali pia viongozi mbalimbali waliofanya ziara ya kukagua shule hiyo ambayo ilijengwa kwa makusudi ya kuwapunguzia wanafunzi mwendo mrefu wa kilomita 14 wanaotembea kwenda kusoma shule ya msingi Ujuni iliyopo kijiji cha jirani cha Ujuni

Mbali na shule hiyo kuwa na vyumba viwili vya madarasa, chuma kimoja wanasomea wanafunzi wa darasa la tatu na la nne kwa kuchanganywa pamoja, na chumba kimoja wanatumia darasa la tano tu peke yao

Hayo yamebainika baada ya ziara ya mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula kufanya ziara katika shule hiyo kukagua hali ya ujenzi na maendeleo kwa ujumla katika shule hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika kata mbalimbali wilayani hapo

Viongozi hao wa CCM wamezidi kushuhudia maajabu katika shule hiyo kwa kujionea chumba ambacho wanasomea wanafunzi wa darasa la kwanza na la pili kikiwa hakina paa, bati wala sakafu ambapo wakati mwingine waalimu hukifunika kwa turubai ili kuwakinga na jua na wakati wa mvua havitumiki

"kama mnavyojionea ndugu viongozi wa CCM hali ni ngumu kwa kweli, tunaupungufu wa vyumba vitano vya madarasa, watoto wa darasa la kwana na la pili wanasomea kwenye chumba hiki ambacho hakina bati muda wote, wakati wa mvua hakitumiki kabisa, na wote tunawachanganya kwenye chumba hiki kimoja" alisema mwalimu mkuu Hester Mahenge

Viongozi hao ambao walikagua vyumba vyote vya shule hiyo pia waligundua shule hiyo ina upungufu wa madawati 50

Akizungumza shuleni hapo katibu wa CCM wilaya ya Makete Miraji Mtaturu amewapongeza wananchi wa Nkenja kwa kujitoa kwa gharama zao hadi hapo madarasa mawili yanayojengwa yalipofikia, na kuwaomba kushirikiana na kutilia mkazo suala hilo ili ujenzi huo ukamilike ndani ya mwaka huu

Amesema pamoja na wananchi hao kukabiliwa na michango mingi lakini watoe kipaumbele kwa ujenzi huo ili wanafunzi hao wasome kwa raha ukizingatia wanafunzi wanaosomea pagalani ni wa darasa la kwanza na pili ambao ndio wachanga wanaohitaji msaada kwa ukaribu zaidi

Naye mwenyekiti wa CCM wilayani hapo Francis Chaula amewataka kuandika bajeti ya vitu vinavyohitajika na gharama zake ili kukamilisha miradi hiyo na waipeleke kwa mkurugenzi mtendaji wa wilaya na nakala kwa chama chake ili kutilia mkazo zaidi namna ya kuboresha mazingira ya shule hiyo

Diwani wa kata ya Kitulo ilipo shule hiyo Mbosa Tweve amesema serikali kupitia halmashauri ya wilaya kwa bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2014 imetoa sh. milioni 8 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo na muda wowote kuanzia sasa zitapelekwa shuleni hapo na kuahidi kushirikiana kukamilisha ujenzi huo

baadhi ya wananchi wa kijiji hicho wamelalamikia michango ya ujenzi huo kuchangwa na kitongoji kimoja tu ilihali kijiji kina vitongoji vinne na kusema hali hiyo inachangia mradi huo kusuasua, huku hoja hiyo ikijibiwa na mwenyekiti wa kijiji hicho Zablon Chengula kuwa amesawaita wenyeviti wa vitongoji vyote kuzungumzia suala hilo na wapo wananchi ambao wameshapelekwa kwa mtendaji wa kata kushughulikiwa kutokana na kugoma kushiriki zoezi hilo

Shule hiyo ina madarasa matano (I-V) ina jumla ya wanafunzi 51 wanaofundishwa na waalimu watatu tu

No comments

Powered by Blogger.