Header Ads

TAARIFA KWA UMMA;KUWASILI KWA MWENGE WA UHURU SEPTEMBA 4 JIJINI DAR

MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU KATIKA MKOA WA DAR ES SALAAM. 

 Ndugu Wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Napenda nitumie fursa hii kuwafahamisha wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuwa Mwenge wa Uhuru utawasili Mkoani kwetu  kesho tarehe 04/09/2013 ukitokea Mkoa wa Pwani na makabidhiano rasmi yatafanyika pale Airport Terminal 1 saa 3:00 asubuhi. Baada ya makabidhiano Mwenge wa Uhuru utakimbizwa katika wilaya zote tatu kama ifuatavyo;-  

1.Tarehe 04/09/2013 utakimbizwa katika Wilaya ya Kinondoni.
2.Tarehe 05/09/2013 utakimbizwa katika Wilaya ya Ilala.
3.Tarehe 06/09/2013 utakimbizwa katika Wilaya ya Temeke.

Ndugu Wananchi,
Mwenge wa Uhuru katika Mkoa wa Dar es Salaam utazindua, kufungua au kuweka mawe ya Msingi katika miradi 26 yenye jumla ya thamamni ya T.shs. BILIONI 23.2. Mkesha wa Mwenge wa Uhuru utakuwa katika sehemu tofauti tofauti kulingana na Wilaya husika. Katika Wilaya ya Kinondoni Mwenge  wa Uhuru utakesha katika SHULE YA MSINGI BUNJU “A”. Katika Wilaya ya Ilala Mwenge wa Uhuru utakesha katika SHULE YA MSINGI MAJANI YA CHAI. Katika Wilaya ya Temeke Mwenge wa Uhuru utakesha katika VIWANJA VYA ZAKHEM-MBAGALA KUU.
 Ndugu Wananchi.

Ujumbe wa Mwenge mwaka huu unasema WATANZANIA NI WAMOJA TUSIGAWANYWE KWA MISINGI YA TOFAUTI ZETU ZA DINI, ITIKADI, RANGI NA RASILIMALI. Ujumbe huu umeandaliwa kwa mwaka huu ili kutoa msisitizo juu ya umuhimu wa kuimarisha Umoja na Amani katika jamii yetu.

Sambamba na ujumbe huu suala la Mapinduzi  Matukufu ya Zanzibar litafafanuliwa kwa kuzingatia umuhimu wake katika kuenzi historia na maendeleo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia mapambano dhidi ya UKIMWI, Rushwa na Matumizi ya Dawa za kulevya yataendelea kusisitizwa. Ujumbe huu utatolewa katika maeneo mbalimbali katika Wilaya zote tatu hususani katika mkesha wa Mwenge.
 Ndugu Wananchi,

Kila eneo ambalo Mwenge umepangiwa kuzindua miradi au kuweka mawe ya msingi patatolewa ujumbe mahsusi wa Mwenge na Kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa Ndugu Juma Ali Simai kama ilivyo desturi nawaomba mjitokeze kwa wingi kuulaki Mwenge wetu wa Uhuru katika maeneo yote.
  Ndugu Wananchi,

Mwenge wa Uhuru utamaliza mbio zake hapa Mkoani tarehe 07/09/2013 na utakabidhiwa kwa uongozi wa Mkoa wa Lindi katika Uwanja wa Ndege wa Kilwa Masoko saa 3:00 asubuhi.
 Ndugu Wananchi,

Napenda nitoe wito kwa wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge wetu wa Uhuru kama ilivyo desturi yetu kwa Utulivu, Amani, Umoja na Mshikamano na kushiriki kikamilifu katika maeneo yote tuliyopanga kuzindua miradi na kuweka mawe ya msingi.

IMETOLEWA NA 
Saidi Meck Sadiki
Mkuu wa Mkoa
DAR ES SALAAM
03/09/2013

No comments

Powered by Blogger.