Header Ads

PICHA: Michezo ya SHIMIWI ilivyofunguliwa mkoani Dodoma

 Hatimaye mashindano ya michezo ya SHIMIWI yanayoshirikisha watumishi wa Serikali kutoka Wizara,Idara Zinazojitegemea,Ofisi za Mikoa na Taasisi za Umma yamefunguliwa rasmi jana katika viwanja vya Jamhuri mjini Dodoma.
Akifungua mashindano hayo mgeni rasmi Naibu Waziri Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mh.Amos Makala aliwataka viongozi wa serikali kuwapa nafasi ya kushiriki mashindano hayo watumishi walio chini yao ili kujenga umoja wa kitaifa,kujenga ari ya ushindani kati ya watumishi na taasisi zake na kujenga afya.
Mh.Makala alisema kuwa ushiriki wa watumishi wa serikali katika michezo unasaidia kujenga urafiki na kuondoa tofauti za udini na ukabila.
Alisisitiza juu ya kuenzi mashindani hayo yenye manufaa kwa watumishi wa umma.
“Ni vema tuyaenzi mashindano ya SHIMIWI kwa hali na mali” alisema Mh.Makala.
Aidha,Mh.Makala aliwataka viongozi kuruhusu kufanyika kwa bonanza za michezo mara kwa mara ili kuwezesha watumishi kubadilishana mawazo na kuendeleza michezo.
Naye Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Bw.Lethy Gembe aliwataka watumishi kuendeleza upendo,undugu,furaha na amani katika kipindi chote cha mashindano hayo.
“Zingatieni ushirikiano na kuheshimiana katika kipindi hiki cha mashindano na hakikisheni mnafuata sheria bila kushurutishwa”alifafanua Bw.Gembe.
Kwa upande wa Mwenyekiti wa SHIMIWI Taifa Bw.Daniel Mwalusamba alisema tangu kuanzishwa kwa mashindano ya SHIMIWI idadi ya ushiriki imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Pia,Bw.Mwalusamba alisisitiza juu ya umuhimu wa waajiri kuhimiza watumishi kushiriki katika michezo.
“Viongozi waendeleze utaratibu wa kukutana kwa njia ya mabonanza ya michezo”alisema Bw.Mwalusamba.
Mashindano ya SHIMIWI yanayohusisha mpira wa pete,mpira wa miguu,kuvuta kamba,bao na karata yanatarajiwa kumalizika Oktoba 5 mwaka huu mjini Dodoma.
 Timu ya Wizara ya Nishati na Madini ikiwa katika maandamano ya ufunguzi wa SHIMIWI katika viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma 
 Timu kutoka Wizara na Idara za Serikali mbalimbali zikimsikiliza mgeni Rasmi,Naibu Waziri Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mh.Amos Makala (hayupo pichani) wakati wa ufunguzi wa michezo ya SHIMIWI Mkoani Dodoma
 Bunge Sports Club nao walikuwepo
 Kaimu Mkuu wa Mkoa Dodoma Bw.Lethy Gembe akitoa hotuba wakati wa ufunguzi wa michezo
 Mwenyekiti wa SHIMIWI Bw.Daniel Mwalusamba akimkaribisha mgeni rasmi
Mgeni rasmi Naibu Waziri Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Mh.Amos Makala akifungua rasmi michezo ya SHIMIWI ya mwaka huu katika Viwanja vya Jamhuri Mkoani Dodoma leo mchana.

No comments

Powered by Blogger.