Header Ads

MKUU WA MAJESHI JENERAL MWAMUNYANGE AWATUNUKU NISHANI MAAFISA WA JESHI ZANZIBAR

Na Amina Abeid (ZJMMC)  .

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ) Jenerali Davis Adolf Mwamunyange leo amewatunuku Nishani Maafisa na Askari 39 wa JWTZ katika hafla iliyofanyika Kambi ya Jeshi ya Bavuai nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Mwamunyange amefanya zoezi hilo kwa niaba ya Rais wa Jamuhuri wa Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na kufanya Idadi ya Wanajeshi waliotunikiwa Nishani msimu huu kutimia 939 Tanzania kwa ujumla.

Zoezi hilo limefanyika kwa Maafisa na Askari Jeshi wenye sifa za kulitumikia Jeshi kwa muda mrefu na kwa tabia ya kuweza kusifika katika Jeshi hilo.

Katika Zoezi hilo Maafisa wawili walitunikiwa Nishani ya Utumishi uliotukuka, Maafisa sita Wametunukiwa Nishani ya muda mrefu ambapo  Askari 31 wametunukiwa nishani ya tabia njema.

Akifafanua kuhusu Nishani hizo Mwamunyange amesema Nishani ya Utumishi uliotukuka hutolewa kwa Maafisa wenye cheo cha Meja kwenda juu ambao wametumikia Jeshi kwa miaka isiopungua 20 mfululizo.

Amesema Nishani ya Utumishi mrefu hutolewa kwa Maafisa na Askari wa JWTZ ambao wametimiza utumishi usiopungua miaka 15 mfululizo na nishani ya Utumishi mrefu na tabia njema huvishwa Askari wa JWTZ waliotumikia Jeshi mfululizo kwa muda usiopungua miaka 15.

Mkuu huyo wa Jeshi amesema Utaratibu huo wa kutunuku nishani umekuwa ukifanywa kwa muda mrefu kwa lengo la kupata Viongozi na Makamanda bora wa Jeshi ambao wametumikia Taifa lao kwa uaminifu na uzalendo wa hali ya juu.

Kwa upande wake mmoja wa Watunukiwa wa Nishani ya Utumishi wa Muda mrefu na tabia njema Saida Said amesema, amefarajika kupata nishani hiyo kwani itamtambulisha Jeshini kuwa ana tabia njema.
Zoezi la kutunuku nishani kwa Maafisa na Askari wa JWTZ limefanyika katika kituo cha KJ 12,Zanzibar na linatarajiwa kuendelea kwa vituo vingine nchi Nzima.
IMETOLEWA NA MAELEZO ZANZIBAR.

No comments

Powered by Blogger.