Header Ads

WIZARA YA MALIASILI NA UTALII YAKANUSHA UVUMI KUWA WATEULE WA WAZIRI WAMESAINI POSHO MBILI


JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALI
  
TAARIFA KWA UMMA
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII IMEKANUSHA UVUMI KUWA WATEULE WA WAZIRI WAMESAINI POSHO MBILI.

Wizara ya Maliasili na Utalii  inakanusha uvumi ulioandikwa na kuchapishwa na gazeti la Raia Mwema mnamo tarehe 07/08/2013 ukurasa wa kwanza lililobeba kichwa cha habari UFISADI kama wabunge, wateule wa waziri wasaini posho mara mbili  ikiwa na ufafanuzi kuwa yumo Ofisa Takukuru,walipwa na taaasisi wanayoichunguza. Taarifa hii ilikuwa na muendelezo zaidi ukurasa wa tatu wa gazeti hilo.

Wizara inasisitiza kuwa uvumi huo siyo kweli kutokana na sababu zifuatazo:
·        Wajumbe wa kamati husika (iliyoundwa kuchunguza tuhuma kuhusu matumizi mabaya ya fedha unaowahusisha watendaji wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro) (NCAA) HAWAKULIPWA POSHO MARA MBILI.

·        Malipo waliyolipwa wajumbe wa kamati husika yalilipwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro  (NCAA) kama ilivyo kwenye Hadidu za Rejea za kazi husika na hawakulipwa malipo yoyote na wizara ya maliasili na utalii.

·        Viwango vya posho vilivyotumika ni kwa mujibu wa Waraka wa Serikali namba 2 wa Mwaka 2010, Ref.Na C/AC/.17/45/01/125

·        Malipo yaliyofanywa kwa wajumbe wa kamati husika yalikuwa na kibali halali cha Waziri wa Maliasili na Utalii Mhe. Khamis Suedi Kagasheki

·        Kamati husika ilifanya kazi vizuri na kukabidhi ripoti ya awali iliyomridhisha Waziri Kagasheki aliyewaagiza kuifanya kazi tajwa hapo juu. Ripoti hiyo ya awali na hii ya mwisho ZITAWEKWA HADHARANI ili Umma uelewe hali halisi ya Mamlaka ya Ngorongoro na siyo upotoshaji wa Raia Mwema.

·        Kamati iliyoundwa na Waziri Kagasheki ilikuwa na kazi tofauti na ile kamati ya awali iliyowahi kuongozwa na Jaji Robert Mihayo aliyeteuliwa na aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige mwaka 2011. Raia Mwema ingejiridhisha kwa kutazama hadudi za rejea za Kamati hizo mbili. Si jambo jema Raia Mwema kuupotosha Umma.

Wizara ya Maliasili na Utalii imesikitishwa na kitendo cha gazeti la Raia Mwema, gazeti ambalo limejijengea sifa na kuaminiwa na jamii kwa  kutoa taarifa  za uhakika zinazofuata maadili ya utoaji taarifa kwa vyombo vya habari, kuchapisha habari zinazochafua jina la Wizara, Wabunge na Serikali kiujumla  bila kujihakikishia ukweli wa taarifa hizo kutoka wizara husika.

Kwa taarifa hii, Wizara inalitaka Gazeti la Raia Mwema kufuta uvumi waliochapisha kwenye gazeti lao kama ilivyotajwa hapo juu na pia kuiomba radhi Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuchapisha habari ambazo si sahihi na pia kuchafua jina la Wizara.

IMETOLEWA NA  KITENGO CHA MAWASILIANO YA SERIKALI
WIZARA YA MALIASILI NA UTALII
12/08/2013

No comments

Powered by Blogger.