Header Ads

SERIKALI KUREJESHA UDHAMINI WA MAFUNZO YA URUBANI

 IMG 3 
  IMG 1 
Mhandisi Mkuu Idara ya Uongozaji Ndege toka Mamlaka ya Usafiri wa Anga Mhandisi Valentina Kayombo (kushoto) akielezea kwa waandishi wa habari(hawapo pichani) mpango wa Mamlaka hiyo kutumia zaidi ya bilioni 3.8 kwa ajili ya kununulia mitambo miwili ya kisasa ya kuongozea ndege, kulia ni Afisa Habari wa mamlaka hiyo Bestina Magutu. 
 
………………………………………………

Picha zote na Eliphace Marwa
Katika jitihada za kuijengea uwezo sekta ya usafiri wa anga nchini Serikali kupitia Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania(TCAA) kuanzia mwaka wa fedha wa 2013 imeanza tena kutoa udhamini  kwa mafunzo ya marubani nchini lengo ikiwa ni kuhakikisha  nchi inakua na marubani wazalendo wakutosha. 

Udhamini huo unatoka katika mfuko wa mafunzo wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga, unaosimamiwa na kanuni ya mwaka 2007 inayofahamika kama “Civil Aviation (Contribution and Administration of Training Fund)” ambao umenza kufanya kazi rasmi mwaka 2011.

Kupitia mfuko huo jumla wanafunzi watano watapata fursa ya kugharimiwa mafunzo ya urubani nchini Afrika Kusini katika chuo cha 43rd Air School kwa muda wa miezi 14, ambapo ada ya mafunzo kwa kila mwakafunzi ni zaidi ya Dola za Kimarekani elfu 62 .

Zaidi ya Dola za Kimarekani laki mbili zimekusanywa kwa ajili ya kuendesha mfuko huo hadi sasa, fedha ambazo zinaendelea kukusanywa kutoka kwa wadau mbali mbali wa usafiri wa anga.

Jumla ya watu 272 waliomba udhamini wa mafunzo hayo, baada ya mchujo wa kwanza yaani (Aptitude Test), wanafunzi 85 walifanikiwa kuingia kwenye awamu ya pili ya mchujo na baada ya kufanyiwa uchunguzi wa kiafya wanafunzi 11 walifanikiwa kuingia kwenye awamu ya mwisho ya usahili iliyofanyika 14 /08/2013 kwa ajili ya kupata wanafunzi watano watakaopata udhamini huo.

Wanafunzi hao watano wanatarajiwa kuanza masomo yao ya urubani muda wowote kuanzia sasa.

Wakati huo huo, Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) itatumia zaidi ya  Bilioni 3.2 kwa ajili ya kununulia mitambo miwili ya kisasa  ya kuongoza ndege hatua ambayo imelenga kuboresha huduma hizo pamoja na hali ya usalama katika anga la Tanzania.

Kampuni ya Ujerumani ya COMSOFT imepata zabuni ya mradi huo utakaohusisha ufungwaji wa mtambo wa  seteliti wa kufuatilia vyombo angani(Survillence) wa ADS-B yaani Automated Data Surveillance-Broadcast unaogharimu Euro 959,490,000 na ule wa kukusanya na kutuma taarifa za usafiri wa anga wa AMHS yaani Aeronautical Massage Handling System unaogharimu Euro 621,345,256.
      
Utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza wakati wowote, baada ya kukamilika kwa taratibu zote za manunuzi na unatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka kesho Utakapokamilika mtambo huo wa ADS-B utawezesha waongoza ndege kufuatilia mwenendo wa vyombo vinavyopita angani katika eneo lote la Mashariki mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na bahari ya Hindi.

Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania imechukua hatua hiyo ili kwenda sanjali na mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya usafiri wa anga lakini pia kumudu ongezeko la safari za anga  hatua ambayo inalazimu kuimarisha miundombinu ya kuongozea ndege.

Tanzania itakuwa miongoni  mwa nchi chache barani Afrika zitakazoanza kutumia teknolojia hiyo ya kisasa ya ADS-B  pale mradi utakapokamilika.

No comments

Powered by Blogger.