Header Ads

MRIPUKO WA BOMU WAWAUA WATU 18 BEIRUT

Mripuko mkubwa wa bomu la kutegwa katika gari umeripuka mjini Beirut nchini Lebanon na kuwaua watu 18 na kwajeruhi wengine zaidi ya 200 katika eneo lililo na watu wengi ambayo ni ngome ya kundi la wanamgambo la Hezbollah.

Kundi ambalo halikuwa linajulikana hapo awali la Syria linaloaminika kuwa na mafungamano na waasi wanaotaka kumng'oa madarakani Rais wa Syria Bashar al Assad limekiri kuhusika na shambulio hilo lililotokea jana jioni.

Shirika la msalaba mwekundu nchini Lebanon limesema watu 18 wameuawa na wengine 245 wamejeruhiwa katika shambulio hilo lililoteka kati ya mitaa ya Bir al Abed na Rweiss kusini mwa mji mkuu.

Shambulio hilo lilisababisha uharibifu mkubwa wa majengo na kusababisha moto ulioteketeza magari kadhaa huku moshi mkubwa ukionekana kufuka kutoka eneo hilo.

Gharama ya kujihusisha na mzozo wa Syria
Mripuko huo unakuja siku moja tu baada ya kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah kusema kundi lake linachukua hatua za kuhakikisha usalama katika eneo hilo la kusini baada ya shambulio jingine la bomu mwezi uliopita katika eneo la Bir al abed kusababisha vifo vya watu kadhaa.

  Gari lililoharibiwa katika mripuko wa bomu Beirut,Lebanon
 
Aliyeshuhudia mripuko huo wa jana alisema aliona gari moja likizunguka eneo hilo mara tatu kabla ya dereva wa gari hilo kupata sehemu ya kuliegesha na kuliripua.Mpiga picha wa shirika la habari la Afp alisjhuhudia miili iliyochomeka vibaya na magari kadhaa yakiteketea.

Vikosi vya usalama vya Hezbollah vimepelekwa katika eneo la mkasa.Hezbollah inamuunga mkono Rais Assad katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Syria na mwaka huu imepeleka wapiganaji wake kulisaidia jeshi la Syria kupambana na waasi wanaotaka kumng'oa madarakani Assad tangu mwezi Machi mwaka 2011.

Punde baada ya shambulio hilo, video iliyowekwa mtandaoni iliwaonyesha wanaume watatu waliojificha nyuso zao wakiwa wameshikilia bunduki mbele ya bendera nyeupe iliyo na maandishi ya kiislamu.

Mmoja wa wanaume hao wa kundi lijiitalo wafuasi wa Aisha Umm al Muminin alimtaja kiongozi wa Hezbollah nguruwe na kusema shambulio hilo ni ujumbe wao wa pili kwake kwasababu yaonekana bado hajawaelewa.

Ni shambulizi la pili dhidi ya Hezbollah
Shambulio hili linakuja wiki sita baada ya jingine lililofanywa na kundi jingine la wapiganaji wa Syria lililodai ni kulipiza kisasi kwa Hezbollah kushirikiana na Assad ambapo watu 50 walijeruhiwa.Muungano wa waasi wa Syria umelaani shambulizi hilo.

Viongozi wa Lebanon kutoka kila upande wa kisiasa pia wamelaani shambulio hilo la jana na kutangaza leo kuwa siku ya maombolezo nchini humo.Rais Michel Sleiman amesema mashambulizi ya kigaidi yanawalenga walebanon wote na sio tu Hezbollah.

Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah Kiongozi wa kundi la Hezbollah Hassan Nasrallah 
 
Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa Ban Ki Moon amezitaka pande zote za kisiasa nchini humo kuungana alipotoa taarifa ya kulaani mashambulizi hayo.

Baraza la usalama la umoja huo pia lilitoa taarifa na kuwataka walebanon wote kuungana wakati huu ambapo kuna naja ya kuyumbisha udhabiti wa taifa hilo na kuzitaka pande zote za kisiasa kujiepusha na mzozo wa Syria.

Mwandishi:Caro Robi/afp/ap
Mhariri: Josephat Charo

No comments

Powered by Blogger.