Header Ads

MKUU WA MKOA WA RUVUMA KUWA MGENI RASMI KWENYE HAFLA YA MIAKA 25 YA HUDUMA YA MAOMBEZI

Huduma ya Maombezi zatimiza miaka 25 Mkoani Rukwa.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Mheshimiwa Injinia Stella Manyanya, atakuwa mgeni rasmi Jumamosi Agosti 17, 2013 katika Matembezi ya Sala ya kumshukuru MWENYEZI MUNGU kwa Amani tuliyonayo hadi leo katika taifa letu na huduma za Maombezi kutimiza miaka 25 katika mkoa wa Rukwa.

Matembezi haya yameandaliwa na Kituo cha Huduma za Maombezi (Marian Faith Healing Centre) zinazoongozwa na Mtumishi wa Mungu, Rev. Fr. Felician Nkwera; yataanzia Mazwi saa 12.00 asubuhi, kupitia Katandala, Sokoni, Majengo hadi kituo cha Sala za Maombi kilichopo Hillside Majengo Sumbawanga mjini.

Haya ni Matembezi ya kumi ya sala katika mfululizo wa matembezi ya sala ambayo Huduma za Maombezi zimekuwa zikifanya jijini Dar es salaam, Mbeya na Sumbawanga tangu kuanzishwa kwake mwaka 1969. Matembezi ya sala ya tisa yalifanyika Disemba 1, 2012 kuanzia TAZARA hadi kwenye kituo cha Huduama za Maombezi cha Riverside kilichoko eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam. Mgeni rasmi  katika matembezi hayo alikuwa Mheshimiwa Pereira Silima, Naibu Waziri kwa niaba ya Dkt. Emmanuel Nchimbi, Waziri wa Mambo ya Ndani. Takriban watu  3000 walishiriki katika matembezi hayo

Malengo makuu ya matembezi haya ni pamoja na :-:
1.      Kumshukuru MWENYEZI MUNGU kwa amani ambayo tunayo katika Taifa letu hadi leo.
2.      Kumuomba MWENYEZI MUNGU azidi kutulindia amani ya ndani ya Taifa letu na katika mipaka na majirani zetu.

3.      Kumuomba MWENYEZI MUNGU aponye maradhi makubwa yanayolidhoofisha Taifa letu (Rushwa, Ufisadi, Ushirikina na Ukimwi).
Huduma za Maombezi ni utume maalum wa sala za tiba: Yaani uponyaji wa maradhi na kupunga pepo. Haubagui kwa misingi yoyote ile. Ni zawadi kubwa kutoka kwa MWENYEZI MUNGU kwa watu wa Tanzania na ulimwengu mzima. Huduma za Maombezi zimeenea sehemu mbalimbali Tanzania na nchi nyingine za Africa, pia Ulaya, Amerika na Asia.

Watanzania wote mnaalikwa kushiriki katika nafasi hii ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutupatia Huduma za Maombezi pia kuzidi kuliombea Taifa letu amani ya kudumu.
  
Sylivester Shayo

MWENYEKITI, HUDUMA ZA MAOMBEZI

No comments

Powered by Blogger.