Header Ads

MAELFU WAJITOKEZA KUANDAMANA TENA MISRI


Waandamanaji Misri
Maelfu ya wafuasi wa Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani Mohammed Morsi wameanza maandamano mengine mjini Cairo, huku kukiwa na hofu ya kuzuka makabiliano zaidi. 

Maafisa wa usalama wamezingira barabara kuelekea medani ya Ramses ambapo maandamano hayo yalipangwa kufanyika. Maandamano ya sasa yanajiri siku mbili baada ya jeshi kuvunja kambi ambapo wafuasi wa vuguvugu la Muslim Brotherhood walikua wamesalia kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Makabiliano yalizuka na zaidi ya watu 600 wakauawa, maelfu walijeruhiwa.Maandamano zaidi yanaendelea nje ya mji mkuu Cairo na taarifa zinasema watu wanne wameuawa kwenye makabiliano eneo la Ismailia. Polisi wa Misri wameamrishwa kutumia risasi za moto kulijinda na kulinda majengo ya serikali dhidi ya kushambuliwa.

Huku utawala wa mpito ukitangaza hali ya hatari, mwandishi wa BBC aliyeko Cairo amesema taharuki imetanda mji mzima.Maelfu walikusanyika nje ya msikiti mmoja baada ya Muslim Brotherhood kuwaomba wafuasi wao kuandamana baada ya sala ya ijumaa wakiitaja kama siku ya hasira. 


Magari ya kijeshi yanashika doria mjini Cairo, na njia ya kuingia medani ya Tahir kitovu cha maandamano ya mwaka 2011 yaliyomuondoa madarakani Hosni Mubarak imefungwa. 

Huku haya yakiarifiwa wapinzani wa Mohammed Mosri pia wamepanga kuandamana dhidi ya mahasimu wao. 

Wakati huo huo watu wameombwa kulinda makaazi yao, makanisa na biashara. Wakristo nchini Misri wamekuwa wakilengwa katika siku za karibuni na makundi ya kiisilamu yenye misimamo mikali. Jumla ya makanisa 25, makaazi na biashara yalishambuliwa hapo Jumatano na Alhamisi.

No comments

Powered by Blogger.